• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Raha ya watahiniwa wa KCSE 2023 masomo ya lazima yakipunguzwa

Raha ya watahiniwa wa KCSE 2023 masomo ya lazima yakipunguzwa

Na DAVID MUCHUNGUH

ZAIDI ya wanafunzi milioni tano watafaidi kutokana na mfumo mpya wa uorodheshaji wanafunzi katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) utakaozingatia masomo waliopita vizuri pekee katika ukadiriaji wa gredi yao ya mwisho.

Katika mfumo huo mpya, masomo ambayo wanafunzi hao wamepata alama duni hayatazingatiwa wakati wa ukadiriaji wa gredi yao ya mwisho.

Chini ya mfumo huo uliotangazwa jana na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu Jumatatu Septemba 25, 2023, masomo ya lazima yamepunguzwa kutoka matano hadi mawili.

Gredi ya wastani ya watahiniwa itakadiriwa kwa msingi wa masomo mawili (Hisabati na lugha moja- Kiingereza, Kiswahili au Lugha ya Ishara), na masomo mengine matano ambayo mtahiniwa amepata alama za juu.

Mfumo ambao umekuwa ukitumika hadi kwa watahiniwa wa KCSE ya mwaka wa 2022, umekuwa ukizingatia masomo sita ya lazima (Kiingereza, Kiswahili, Hisabati na masomo mawili ya Sayansi) na mawili ya Sanaa.

Mfumo huo haukuwafaa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ambayo hayako ndani ya orodha hii ya masomo ya lazima.

“Inatarajiwa kuwa mabadiliko haya yataongeza idadi ya wanafunzi wanaohitimu kujiunga na vyuo vikuu, vyuo vya kadri, vya kiufundi (TVET) na vya ngazi ya vyeti,” Bw Machogu akasema jana.

Alikuwa akiongea katika Makao Makuu ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) alipozindua msimu wa mitihani ya mwaka huu wa 2023.

Kulingana na jaribio lililoendeshwa na KNEC kwa kuzingatia alama za watahiniwa wa KCSE 2022, ikiwa mfumo huu mpya ungetumika, jumla watahiniwa 199,929 wangepata gredi ya C+ kwenda juu (asilimia 22.79).

Hii ni tofauti na watahiniwa 173,345 (asilimia 19.62) waliopata gredi ya C+ kwenda juu chini ya mfumo zamani.
Jumla ya watahiniwa 903,260 wamesajiliwa kufanya KCSE mwaka huu.

Mabadiliko hayo ni sehemu ya mapendekezo ya ripoti ya Jopokazi la Rais kuhusu Mageuzi katika Elimu.

  • Tags

You can share this post!

Kiwanda cha sukari chalilia wakulima wapeleke miwa ili...

Kinyesi cha binadamu chatumika kuzuia MCAs kumbandua gavana...

T L