• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 3:55 PM
Kiwanda cha sukari chalilia wakulima wapeleke miwa ili kisisambaratike

Kiwanda cha sukari chalilia wakulima wapeleke miwa ili kisisambaratike

KNA na LABAAN SHABAAN

Huenda Kiwanda cha Sukari cha South Nyanza (SONY) kikafungwa kwa sababu ya kukosa miwa ya kutosha kwani huchakata miwa mara moja kwa juma kinyume na kila siku hapo awali.

Inabidi usimamizi wa SONY ukusanye miwa kutoka kwa wakulima kila siku hadi wafikie viwango vya kuwasha mashini ili kuzalisha sukari.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya SONY Bw Jared Kopiyo amesema shughuli ya kukusanya miwa kwanza na baadaye kuanza kusaga ni kupoteza muda na huchelewesha uzalishaji wa sukari na kuzuia kampuni hiyo kujenga msingi dhabiti wa kulipa madeni na mishahara.

“Inasikitisha kwamba tunalazimika kuzima mashini kwa wiki moja tukisubiri wakulima watuletee miwa kabla ya kuwasha tena,” alisema Bw Kopiyo ambaye awali alikuwa Mbunge wa Awendo.

“Kama wakulima hawatafanya hima kutuletea miwa, tutafunga hiki kiwanda ambacho kilikuwa kinazalisha sukari kila siku,” aliongeza.

Mwenyekiti wa bodi ya SONY ameeleza kiwanda hicho kina malimbikizo ya madeni ya mabilioni ya pesa katika kipindi cha miaka mitatu kwa sababu ya kushuka kwa biashara.

Bw Kopiyo amesikitika kuwa mashini ziko katika viwango vizuri lakini hakuna miwa ya kusaga.

Ili kufufua operesheni ya kiwanda hiki, Mkurugenzi Msimamizi Bw Stephen Ligawa amedokeza SONY iko makini kuendeleza mpango wa ustawishaji wa kilimo cha miwa kuhakikisha kuwa miezi michache ijayo, kiwanda kitapokea miwa kutoka kwa wakulima wake wa mkataba na zaidi.

“Tunatia bidii ili madeni ya wakulima na wasambazaji yapungue kabisa kufikia mwisho wa mwaka,” alisema Bw Ligawa.

  • Tags

You can share this post!

Mkono wa vidume wa kisiasa kwenye masaibu ya Kawira

Raha ya watahiniwa wa KCSE 2023 masomo ya lazima...

T L