• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 9:49 AM
Raila, Sakaja kifua mbele kura zikinukia

Raila, Sakaja kifua mbele kura zikinukia

NA MARY WANGARI

MWANIAJI urais kwa tikiti ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga na mgombea mwenza wake Martha Karua, wanaongoza kwa umaarufu katika Kaunti ya Nairobi, utafiti mpya umeonyesha.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na shirika la Infotrak iliyotolewa Jumatano inaonyesha kuwa, Kiongozi wa ODM na mwenzake Bi Karua wako kifua mbele kwa asilimia 49.

Naibu Rais William Ruto anayeongoza kambi ya Kenya Kwanza katika kinyang’anyiro cha ikulu pamoja na mgombea mwenza wake, Rigathi Gachagua, wanafuatia kwa asilimia 30.

Kiongozi wa Roots Party, George Wajackoya na mgombea mwenza wake, Justina Wamae ambao wameonekana kuzidi kujitwalia umaarufu katika siku za majuzi wanafuata kwa asilimia tano.

Muungano wa Azimio One Kenya unaongoza miongoni mwa kambi za kisiasa kwa umaarufu katika Kaunti ya Nairobi kwa asilimia 51 ukifuatiwa na Kenya Kwanza (31).

Katika siku za majuzi, umaarufu wa Naibu Rais na mgombea mwenza wake, Bw Gachagua umeonekana kuzidi kudorora huku wapinzani wao, Bw Raila na Bi Martha na Bw Wajackoya wakizidi kupanda.

Wachanganuzi wa siasa wamehoji kwamba matatizo ya Bw Ruto yalianza pale tu alipomteua Bw Gachagua na kumtaja rasmi kama mgombea mwenza wake katika kinyang’anyiro cha ikulu.

“Kwa kumteua Bi Karua, Bw Odinga alifikia mawanda mapya ya wapiga kura ambao hajawahi kuwafikia hapo awali. Bi Karua alipuliza uhai mpya katika kambi ya Azimio. Kama wakili na mwanasiasa mwenye tajriba ndefu, anawiana vyema zaidi na Wakenya wa kawaida na pia anavutia kura ya wanawake wanaohisi kuwakilishwa,” anafafanua Bw Mark Bichachi.

“Kwa upande wake, Ruto hakufanya lolote jipya kwa sababu alimchagua mwanasiasa mwenye sifa zilezile ambazo Wakenya wamezoea. Gachagua pia amekuwa akitoa matamshi kiholela yanayoonyesha uhalisia wa matabaka ya kijamii nchini,” alisema.

Huku akipuuzilia mbali kasumba kuwa kiongozi wa Roots Party, ni mradi wa serikali wa kutawanya kura za Naibu Rais, Bw Bichache alisisitiza kuwa Wakenya wamekuwa wakitamani mageuzi, jambo ambalo Bw Wajackoya amewaahidi kupitia manifesto yake.

“Manifesto ya Ruto ni nukuu tu ya Ajenda Nne Kuu ambayo imekuwepo kwa miaka kadhaa. Wajackoya anawapa Wakenya matumaini mapya ya mageuzi yatakayofufua uchumi kama vile ufugaji wa nyoka, ukuzaji wa bangi ya kuuzwa katika mataifa ya kigeni na mengineyo. Wajackoya pia anavutia mahasla ambao wanalengwa na Dkt Ruto,” alieleza.

Kuhusu kiti cha ugavana Nairobi, utafiti huo uliofanyika katika maeneobunge 17 na wadi 85 Kaunti hiyo unaonyesha kuwa Seneta Johnstone Sakaja anayewania kwa tiketi ya UDA ndiye maarufu zaidi kwa asilimia 39. Mshindani wake mkuu, Bw Polyarp Igathe anafuatia kwa asilimia 33 na Bi Agnes Kagure asilimia 0.4.

  • Tags

You can share this post!

Siku ya Kiswahili Duniani yaadhimishwa kwa njia ya kipekee...

TAHARIRI: Magavana wajao watii sheria za ugatuzi kuhusu...

T L