• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
TAHARIRI: Magavana wajao watii sheria za ugatuzi kuhusu mgao wa pesa

TAHARIRI: Magavana wajao watii sheria za ugatuzi kuhusu mgao wa pesa

NA MHARIRI

RIPOTI ya hivi punde ya Mkaguzi wa Bajeti inaonyesha kaunti 42 zilitumia mabilioni ya pesa kwa mishahara badala ya maendeleo.

Hata zile zilizojaribu kufadhili maendeleo, ufadhili huo haukupita asilimia 25 (robo) ya pesa zote zilizowasilishwa na wizara ya Fedha.

Ikilinganishwa na mwaka uliopota, mwaka huu kaunti zilitumia Sh40 bilioni zaidi kwa mishahara na marupurupu. Jambo hili bila shaka liliathiri jinsi ambavyo kaunti zilitekeleza maendeleo.

Kaunti tano; Taita Taveta, Nairobi, Narok, Kiambu na Machakos ndizo zilizokiuka mipaka katika kuwanyima wananchi maendeleo. Kwa mfano, kati ya mabilioni ambayo kaunti hiyo ya Gavana Granton Samboja ilipewa, ilitumia asilimia 2.7 pekee kwa maendeleo.

Taita Taveta ni kati ya kaunti zinazokumbwa na changamoto nyingi, ukiwemo umasikini wa hali ya juu. Kutumia Sh84 milioni kwa maendeleo ni jambo linalozua wasiwasi.

Nairobi ilitumia Sh15.2 bilioni kwa mishahara na matumizi mengine yasiyo ya maendeleo, lakini Sh1 bilioni pekee kwa maendeleo. Mishahara pekee ilikuwa zaidi ya mara kumi ikilinganishwa na pesa zilizotumiwa katika maendeleo.

Kaunti hizo hazikuona ubaya wowote wa wasimamizi kujali maslahi yao kuliko huduma kwa wananchi.

Matumizi kulipia mishahara, marupurupu na mengine yasiyo ya maendeleo kama matumizi ya ofisini, yaliongezeka kutoka Sh172.9 bilioni hadi Sh212.9 bilioni, ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka jana. Hata hivyo, matumizi kufadhili miradi ya maendeleo yalipungua kutoka Sh48.45 bilioni hadi Sh44.3 bilioni.

Hali ilikuwa hivyo katika kaunti nyingine nyingi. Pesa zinazosambazwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) zinatumiwa kwa matumizi yasiyokuwa na faida ya moja kwa moja kwa mwananchi .

Sheria inasema pesa za mishahara na matumizi mengine zapaswa kuwa asilimia 70 na asilimia 30 iwe ya maendeleo.

Kinachosababisha sheria hii kupuuzwa ni uchu wa magavana kuajiri jamaa na marafiki zao kwenye kaunti. Haiwezekani kwa kaunti kuajiri maelfu ya watu kwenye idara mbalimbali. Magavana wengine, kwa kuogopa kulemewa na MCA, huwapeleka kwenye safari za kifahari kutumia pesa ya mwananchi.

Magavana watakaochaguliwa Agosti 9 wanapaswa kujua kuwa, sababu ya Wakenya kutaka ugatuzi, ni ili maendeleo yawafikie kokote waliko.

Ni sharti wanaotaka ugavana waelewe kuwa lengo la uongozi ni utoaji huduma.

You can share this post!

Raila, Sakaja kifua mbele kura zikinukia

WANDERI KAMAU: Wataalamu wetu wafanye bidii kuvumisha...

T L