• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Sakaja na Kihika wamulikwa kwa ‘kudharau’ Seneti

Sakaja na Kihika wamulikwa kwa ‘kudharau’ Seneti

NA MARY WANGARI

SENETI imewaamuru magavana wawili kufika mbele yake kwa kile inachotaja kama kukosa heshima na kudharau kamati za Seneti zinazosimamia matumizi ya fedha za umma katika kaunti.

Haya yamejiri huku magavana waliokuwa maseneta wakimulikwa kwa mtindo wao wa kudunisha kamati za seneti. Magavana Johnson Sakaja wa Nairobi na Susan Kihika wa Nakuru wameagizwa kufika mbele ya Kamati ya Seneti inayosimamia Matumizi ya Fedha za Umma na Hazina Maalum.

Hii ni baada ya viongozi hao wanaohudumu kama magavana kwa mara ya kwanza, kukaidi mara kadhaa mialiko ya Seneti ili kujibu maswali kuhusiana na changamoto zinazokabili kampuni za maji katika maeneo yao mtawalia.

Aidha, wakuu hao wa kaunti wameshutumiwa kwa kutoa vijisababu vya uongo na kutumia safari katika mataifa ya kigeni kukwepa vikao vya Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Kaunti ya Vihiga, Godfrey Osotsi.

Gavana Sakaja alisusia kikao cha Kamati hiyo jana Jumatatu asubuhi akisema kwamba amesafiri nje ya nchi hata baada ya kuonekana akihudhuria mechi kati ya Gor Mahia na AFC Leopards iliyochezewa katika uwanja wa Nyayo, Jumapili.

Hii ni mara ya tatu Bw Sakaja amekaidi mwaliko wa kufika mbele ya Seneti kujibu maswali yaliyozuka kwenye ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuhusu changamoto ambazo zimehangaisha Kampuni ya Maji na Majitaka Nairobi (NCWSC) kwa zaidi ya miaka mitano.

Kabla ya kuchaguliwa kuwa gavana katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 2022, Bw Sakaja alikuwa seneta ambapo alihudumu pia kama mwenyekiti wa kamati ya Seneti.

“Mara ya kwanza aliomba udhuru akisema anashughulikia suala la kifamilia. Alikuja kikao cha pili ila akasema ana jambo la dharura hivyo tukamilishe mapema. Kikao cha leo kilikuwa kitukamilishie maswali ya awali kuhusu ukaguzi wa fedha za umma. Lakini akatutumia barua ambayo imetiwa saini na kaimu katibu wa kaunti,” alisema Seneta Osotsi.

“Gavana alionekana kupitia runinga ya kitaifa akiwa sehemu ya mashabiki waliohudhuriwa mechi pamoja na Rais na hata kiongozi wa upinzani. Kisha anasema alikuwa nje ya nchi. Tulitarajia awe mfano mwema kwa sababu aliwahi kuwa seneta vilevile.”

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alirejelea barua iliyotumwa na Gavana Sakaja mnamo Ijumaa, Mei 12, 2023 lakini iliyoandikwa Mei 15,2023.

Gavana Kihika vilevile hakujitokeza kwa mara ya tatu mbele ya Kamati hiyo huku barua iliyoandikwa na kutiwa saini na kaimu katibu wa Kaunti ya Nakuru, ikisema amesafiri nje ya nchi.

Kulingana na Seneta Osotsi, magavana hao hawakujibu simu zake licha ya kuwapigia mara kadhaa.

“Tumetoa amri kwa magavana hao kufika mbele ya kamati hii katika tarehe itakayotolewa na Katibu la sivyo, tutatumia sheria kuhusu Mamlaka ya Bunge na kuagiza polisi kuwakamata,” alisema Seneta Osotsi.

Kifungu 18 kuhusu Mamlaka ya Kamati za Bunge kinasema kuwa “Bunge au Kamati zake zinaweza zikamwalika mtu yeyote kufika mbele yake kwa sababu ya kutoa ushahidi au habari, karatasi, kitabu, rekodi au nakala walizo nazo au wanazosimamia.”

Aidha, Kifungu hicho kinasema kuwa “Bunge na kamati zake litakuwa na mamlaka sawia na Mahakama Kuu kulingana na Kipengele 125 cha Katiba.

  • Tags

You can share this post!

Yesu wa Tongaren aachiliwa huru

KUKABILI TATIZO: Uvimbe chini ya macho

T L