• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Serikali yaanza kujenga barabara ya lami kuinua hadhi ya mji wa Othaya

Serikali yaanza kujenga barabara ya lami kuinua hadhi ya mji wa Othaya

Na WANGU KANURI

[email protected]

Serikali kupitia Mamlaka ya Ujenzi wa Barabara za Mijini (KURA) imeanza kujenga barabara ya kilomita 12 katika mji wa Othaya. KURA inanuia kuweka lami, mabomba ya kutoa maji na njia za usafiri kwa waendeshaji basikeli na wanaotembea kwa miguu.

Kulingana na KURA, mradi huo unanuia kuinua hadhi ya mji wa Othaya na kuufanya umakinikie kibiashara.

“Barabara hii ina jumla ya barabara sita ambazo zitapitia katika maeneo mbalimbali kama kanisa la Katoliki la Birithia katika barabara ya Gachame, barabara iliyopendekezwa ya KMTC, barabara ya Gatugi- Sewarage-Karima, kituo cha ununuzi cha Kwa Ngechu-Gatugi, shule ya upili ya wasichana ya Othaya na hospitali ya Othaya level 6 na level 4,” ikasema taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Ijumaa.

Bi Doreen Kirima, mhandisi anayesimamia mradi huo, aliwashukuru wakazi kwa eneo hilo kwa kuwaunga mkono wajenzi hivi kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezeka kwa urahisi. Isitoshe Bi Kirima alieleza umuhimu ambao barabara hiyo italeta pindi tu itakapomalizika.

“Barabara hizo zinajengwa ndani ya mji wa Othaya zitasaidia pakubwa wakaazi kupata kwa urahisi sana huduma katika shule, hospitali na sokoni,” akasema.

Mradi huu ambao umedhaminiwa na serikali utachukua jumla ya miaka miwili ili uweze kukamilika na utatumia Sh474,712,844.76 milioni. Kampuni ya Benisa ndiyo iliyopewa kandarasi ya ujenzi huo na ilianza kujenga barabara hiyo mwaka jana.

Pindi tu mradi huu utakapomalizika, wakaazi wataweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kupunguza muda wa kusafiri na pia kupokea huduma mbalimbali kwa urahisi. Kazi hii ya ujenzi inaambatana na utekelezwaji wa Ruwaza ya 2030 na Ajenda Nne Kuu.

You can share this post!

Wito mashirika yashirikiane kueneza bayoteknolojia nchini

Wenye jinsia mbili walia kubaguliwa wakisaka huduma