• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
Serikali yaombwa kuwaondolea raia mzigo wa gharama ya juu ya maisha

Serikali yaombwa kuwaondolea raia mzigo wa gharama ya juu ya maisha

NA LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya serikali kuangazia na kutatua changamoto ya hali ngumu ya maisha ambayo Wakenya wanapitia baada ya bei za bidhaa za petroli kupanda na utata wa karo ya juu katika vyuo vikuu.

Askofu wa kanisa la Glory Outreach Assembly Church la Kahawa Wendani, David Munyiri Thagana, alisema masomo ya juu yamekuwa ghali kwa wanafunzi wengi waliofuzu.

Aliyasema hayo mnamo Jumamosi alipowahamasisha vijana wapatao 100 wengi wao wakiwa mayatima waliokuwa chini ya ulezi wake.

Vijana hao ambao wanatarajia kujiunga na vyuo tofauti vya masomo walijumuika katika kanisa lake huku wakipokea ushauri jinsi ya kuepukana na majaribu ya kiulimwengu.

Kanisa la Glory Outreach Assembly litawapa wanafunzi hao Sh8,000 za matumizi kwa kila mmoja wao baada ya kulipiwa karo ya masomo.

Askofu alisema kanisa lake linatumia mamilioni ya fedha kugharimia vijana hao.

Askofu Thagana alitoa tahadhari kwa wanafunzi wawe makini wanapojumuika na wenzao vyuoni kwa sababu huko kuna mitego mingi.

Alisema vijana hao wanapata mafunzo ya kidini katika kanisa lake ili wawe na maadili mema yatakayowapa mwongozo wa kuwa Wakristo waaminifu.

Wanafunzi wakipewa ushauri nasaha katika kanisa la Glory Outreach Assembly Church la Kahawa Wendani mnamo Septemba 16, 2023. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Kulingana na Askofu huyo kuna maswala ya ushoga ambayo yameleta mjadala mkali nchini.

Aliwashauri vijana hao wawe makini wasinaswe na mtego huo kwa sababu “sisi Waafrika tuna maadili  na utamaduni wetu ambao tumezoea.”

Alisema maswala ya ushoga ni ya kuangamiza kizazi chetu cha siku zijazo.

“Ninawashauri vijana hao wasije wakaingia kwenye mtego huo ambao utaathiri utu wao,” alisema mchungaji huyo.

Bi Beatrice Otieno ambaye ni mshauri wa maswala ya kijamii, na mhadhiri, aliwashauri vijana kujiamini kwa kujiepusha na maovu.

Aliwashauri vijana kujiepusha na ukasuku wa kuiga wenzao bila kupima.

“Iwapo unataka kuwa na maisha mema, acha kuigiza mwenzako na ufanye kile ambacho kinakufaa kibinafsi,” alishauri Bi Otieno.

Aliwashauri vijana hao kuteua baadhi ya marafiki wanaoshirikiana nao.

Aliwashauri kutopotoshwa na mambo wanayoyaona kwenye mitandao ya kijamii.

“Hata ingawa tunatumia simu za kijiditali lakini tuwe makini kutathmini mambo yale yako mle ndani,” alieleza mshauri huyo.

Alisema simu za rununu zina madhara yake na kwa hivyo vijana wawe chonjo wanapowasiliana na marafiki ama wapendwa wao.

Bw Anthony Ndwiga na Mary Wangui ambao ni vijana wanaojiandaa kujiunga na vyuo vikuu, waliridhika na mafunzo waliyopokea kutoka kwa Askofu Thagana na wataalam wengine.

“Sisi kama vijana chipukizi tumepata ushauri nasaha. Kwa hivyo ni sharti tujichunge tunapokwenda katika mazingira tofauti na yale ambayo tumekuwa tumeyazoea,” alisema kijana Ndwiga.

  • Tags

You can share this post!

Wanaraga wa kike wa Kenya wapoteza vibaya dhidi ya Afrika...

Wakazi Ruiru watumia mbinu za kizamani za upishi bei ya...

T L