• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
Wakazi Ruiru watumia mbinu za kizamani za upishi bei ya mafuta ya kukaangia ikipaa

Wakazi Ruiru watumia mbinu za kizamani za upishi bei ya mafuta ya kukaangia ikipaa

NA LABAAN SHABAAN

MAFUTA ya kupikia kiasi cha lita moja yanauzwa kwa Sh250 hadi takriban Sh400 katika maduka makuu eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Haya ni kwa mujibu wa uchunguzi wa Taifa Jumapili katika supamaketi za Leestar, Powerstar na Quickmart.

Mafuta ya kupima yanauzwa kuanzia Sh210 kulingana na wafanyabiashara wa mikahawa wanaouza hususan chipsi na wengine wanaochuuza vyakula mitaani.

“Huku Ruiru bei ya mafuta ni ile ile na sijaona bei ya mafuta kama imeshuka. Kwa kweli gharama ya maisha iko juu sana,” akasema mkazi wa Ruiru aliyejitambulisha akisema anaitwa Eunice.

Amesema inabidi azoee kupika chakula kwa mbinu za kizamani ikiwemo kuchemsha tu chakula na kuongeza chumvi kwa ladha.

Naye Bw Joshua Nzioka, ambaye ni mchuuzi wa smokies anasema serikali haijajitolea kumfaa Mkenya wa kawaida.

“Awali mafuta yalikuwa Sh100 na kitu na kufikia saa tano asubuhi nilikuwa nikiingiza Sh2,000 lakini siku hizi ambazo gharama ya maisha iko juu, huwa ni vigumu kufikisha Sh1000,” Bw Nzioka akalalamika.

Naye mfanyabiashara mwingine ambaye ni mmilii wa mkahawa, Bi Jane Imai, anaeleza kuwa wateja wao wanalalamikia kuongezeka kwa bei ya vyakula kwa sababu ya gharama ya mafuta ya kupikia.

“Maisha hapa ni magumu kwa sababu ya bei ya mafuta na habari kuwa bei ya mafuta hapa Ruiru ni ya chini ni uvumi na tunaomba serikali ishughulike ili wateja wetu warudi,” anaeleza Imai.

Mhudumu wa teksi mjini Ruiru John Kimani aliyekerwa na bei ya juu ya petroli na mafuta ya kupikia, amelaani hatua ya serikali kupandisha bei za bidhaa muhimu akisema “ninachukia kuchaguliwa kwa viongozi wasiojali maslahi ya raia”.

“Kila kitu kimepanda na kwenda mbele tutakuwa tunakula chakula cha kuchemsha kwa sababu hatuwezi kumudu gharama,” Kimani anasikitika.

Gumzo la gharama ya bei ya mafuta limetamba nchini baada ya Waziri wa Biashara Moses Kuria kudai serikali imepunguza gharama kwa asilimia 50 tangu ilipochukua hatamu za uongozi mwaka wa 2022.

Bw Kuria alisema gharama ya mafuta haya iko chini ya Sh240 hasa eneo la Ruiru takwimu ambazo zimekinzana na bei katika maduka makuu nchini.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaombwa kuwaondolea raia mzigo wa gharama ya juu...

Mung’aro ajiita ‘Binti Kiziwi’ akisema kelele za...

T L