• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Serikali yasema bado inaweka pamoja ushahidi wa kushtaki Pasta Mackenzie na wenzake

Serikali yasema bado inaweka pamoja ushahidi wa kushtaki Pasta Mackenzie na wenzake

NA MAUREEN ONGALA

KATIBU wa Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Raymond Omollo amesema ya kwamba serikali bado inaendelea kufanya uchunguzi wa vifo vilivyotokea katika msitu wa Shakahola.

Dkt Omollo alisema kuwa serikali inatarajiwa kukamilisha uchunguzi huo ndani ya miezi miwili ijayo kisha kuwafungulia mashtaka Pasta Paul Mackenzie na wenzake ambao bado wako kizuizini.

Akihutubia wanahabari katika hoteli ya Ocean Beach mjini Malindi siku ya Alhamisi, katibu huyo alisema kuwa uchunguzi huo umechukuwa muda mrefu kwa sababu miili mingi iliyofukuliwa inafanyiwa upasuaji.

“Kuna miili mingi ambayo tuliondoa kwenye makaburi yaliyofukuliwa huko Shakahola na bado zoezi la upasuaji linaendelea kwani miili mingine ilikuwa imeoza kwa sababu ya kukaa makaburini kwa muda mrefu na hiyo ikatupa changamoto kubwa. Tuko na uhakika tutamaliza ndani ya miezi miwili ijayo,” akasema.

Aliwataka wananchi na familia zilizoathirika kuwa na uvumilivu wakati huu ambapo serikali inashughulikia swala hilo kwa kina.

“Baada ya muda huo tutakuwa tumekamilisha uchunguzi na tutakuwa na ushahidi wa kutosha wa kuwashtaki washukiwa,” akasema.

Maiti zilizofukuliwa Shakahola zinaendekea kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Malindi, alisema.

Mhubiri tata Mackenzie wa Kanisa la Good News International na wafuasi wake bado wanaendelea kuzuiliwa kwa zaidi ya miezi tisa sasa.

Mackenzie inadaiwa aliwashawishi wafuasi wake kuandamana naye hadi ‘jangwani’ katika msitu wa Shakahola ambapo walifunga na baadhi yao wakaanza kufa.

Inadaiwa mafunzo potovu yaliwafanya kuamini kwa kufariki katika hali hiyo, wangeenda mbinguni.

  • Tags

You can share this post!

Waliopigia Azimio wasahau nyadhifa za kuteuliwa, wasubiri...

BAHARI YA MAPENZI: Kushiriki tendo la ndoa bila vijisababu...

T L