• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:39 AM
Waliopigia Azimio wasahau nyadhifa za kuteuliwa, wasubiri tu maendeleo ya kitaifa – Kingi

Waliopigia Azimio wasahau nyadhifa za kuteuliwa, wasubiri tu maendeleo ya kitaifa – Kingi

NA ALEX KALAMA

SPIKA wa Bunge la Seneti Amason Kingi amesuta wanaokosoa kauli za Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba serikali ya Kenya Kwanza ni ya wenye hisa pekee, akisisitiza kwamba waliopigia au kuunga Azimio La Umoja-One Kenya wasahau nyadhifa za kuteuliwa.

Hata hivyo, amesisitiza kwamba serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto itaendelea kuzindua na kufanikisha miradi ya maendeleo katika kila kona ya nchi bila kujali miegemeo ya kisiasa.

Akihutubu katika kijiji cha Isdowe katika Kaunti ya Tana River, spika Kingi alisema kiukweli watu ambao hawakuunga mkono manifesto ya Rais Ruto alipokuwa akiomba kura hawawezi wakamsaidia kutimiza ajenda yake.

“Najua Mheshimiwa Naibu Rais Rigathi Gachagua anasema serikali ya William Ruto ni ya wamiliki wa hisa. anasema ukweli mtupu japo kuna wengine huwa wanapinga anachokisema ila Gachagua huwa anaongea ukweli mtupu. Haiwezekani wakati watu wakiweka kura katika kikapu cha William Ruto wewe uliweka kura katika kikapu kingine halafu wakati wa kuvuna unataka upewe wadhifa. Ni vigumu. Hilo sahau,” akasema spika Kingi.

Kauli hiyo aliitoa katika sherehe ya kuzindua Biblia ya lugha ya Kipokomo.

“Rais Ruto atatekeleza maendeleo katika kila sehemu nchini lakini mambo ya kupewa nyadhifa hilo wasahau. Hata kama ni wewe, huwezi kupatia mtu wadhifa ukijua vyema alikuwa anapinga mpango wako. Baadhi ya watu walikuwa wakipinga kile Ruto alikuwa akiwaambia halafu wao ndio wanataka sijui wapewe nafasi tano za mawaziri sijui nafasi ishirini za makatibu… ni vigumu kwa sababu hawakuwekeza kwake,” akafoka.

Alifananisha hali hiyo na na mtu kuweka sufuria yenye maji kwa moto akitaka kupika halafu mtu mwingine aje apige teke yale maji yamwagike tena.

“Hata Gavana wa Tana River Dhadho Godana hakuwapatia nafasi ya uwaziri katika serikali yake wale ambao walikuwa hawamuungi mkono na hivyo ndivyo ilivyo hata kwa serikali kuu,” akaongeza.

Pia alidai kwamba maandamano ya Azimio yaliyoitishwa na Raila Odinga mapema mwaka 2023 yaliyumbisha mchakato wa kuwapata makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Uchaguzi hauwezi ukafanyika bila tume. Ajenda ya kwanza ambayo tulifanya kama bunge la seneti pamoja na bunge la kitaifa ilikuwa kupitisha sheria ili tume iweze kuundwa. Lakini kwa sababu upande wa upinzani ulileta maandamano ndio maana hadi sasa hatujakuwa na tume,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Vijana waliozoea kula vya haramu kwa uhalifu wasema...

Serikali yasema bado inaweka pamoja ushahidi wa kushtaki...

T L