• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Sonko anaugua maradhi ya ubongo na moyo, hawezi kuendelea na kesi – Mahakama

Sonko anaugua maradhi ya ubongo na moyo, hawezi kuendelea na kesi – Mahakama

Na RICHARD MUNGUTI

RIPOTI ya daktari wa tiba za akili imesema Alhamisi kuwa aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko anaugua maradhi ya ubongo na moyo na kamwe hawezi kuendelea na kesi za ufisadi dhidi yake za uporaji wa Sh24 milioni.

Haya yalijiri huku mahakama ya Kahawa iliyokuwa imeombwa iamuru Sonko azuiliwe kwa siku 30 kuhojiwa na maafisa wa polisi ibainike ikiwa ana mahusiano na matukio ya ugaidi nchini ikimwachilia kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu.

Ufichuzi wa daktari wa matatizo ya akili Pius Kigamwa wa Hospitali za Agha Khan na Nairobi, kwa hakimu mwandamizi mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Milimani Nairobi, Bw Peter Ooko, umefichua kuwa Bw Sonko hana utimamu wa akili, uliopelekea agizo apimwe tena na mtalaam wa maradhi ya ubongo katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) kubaini ukweli.

“Nimesoma kwa ripoti ya Dkt Kigamwa iliyowasilishwa Machi 4, 2021 kwamba Sonko hawezi kuendelea na kesi kutokana na maradhi ya ubongo,” Bw Ooko alisema.

Hakimu huyo alisema pia amesoma kwa makini ripoti nyingine ya madaktari wanne wa KNH iliyosema kuwa Bw Sonko anaugua maradhi ya akili yajulikanayo kwa lugha ya kiutaalam Bipola.

“Kabla ya kutoa uamuzi iwapo kesi dhidi ya Sonko zitaendelea ama zitasitishwa itabidi apimwe tena KNH na daktari wa Serikali abaini ikiwa kabisa gavana huyu wa zamani anaugua ubongo na kamwe hawezi endelea na kesi,” akaamuru Bw Ooko.

Wakili Dkt John Khaminwa anayemtetea Sonko. Picha/ RICHARD MUNGUTI

Bw Ooko alisema akisha pokea ripoti hizo mbili ya Dkt Kigomwa na hiyo ya KNH korti itapata ufahamu kamili kuhusu hali yake. Aliamuru ripoti ya Sonko kutoka KNH iwasilishe kortini Machi 12, 2021.

Hakimu huyo alitoa agizo hilo baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo na Dkt Khaminwa kabla ya kutoa mwelekeo ikiwa kesi ya ufisadi wa Sh14milioni dhidi ya Sonko na washtakiwa wengine wawili ROG Security Limited na Antony Otieno Ombok almaafuru Jamal.

Ombok anawakilishwa na wakili Paula Atukunda. Bw Sonko , ROG na Bw Ombok wameshtakiwa kuporoma pesa za umma kupitia utoaji wa kandarasi ya kuweka stima katika barabara mbali mbali jijini Nairobi.

Dkt Khaminwa alimkabidhi Bw Ooko nakala ya ripoti hiyo ya Dkt Kigomwa na kisha akasema “hii kesi haiwezi endelea nimepokea ripoti kwamba Sonko anaugua maradhi ya ubongo na hawezi endelea na kesi.”

Bw Ooko alisema kuwa ripoti ya madaktari wanne wakuu wa KNH Dkt W K Sigilai, Dkt Bernard Gitura, Dkt Ian Kanyanya na Dkt Phoebe Juma walisema Sonko anaugua maradhi ya akili na “anahitaji tiba ya haraka.”

Mbali na maradhi hayo pia walisema anahitaji kufanyiwa upasuaji wa Nyonga (hip bornes), yuko na presha mbali na magonjwa mengine.

Viongozi wa mashtaka walijaribu kupinga ombi kesi iahirishwe lakini mahakama ikakataa.

Na wakati huo huo hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti alitoroka kusikizwa kwa kesi ya ufisadi wa Sh10milioni dhidi ya Sonko baada ya malumbano makali kuchipuka kati ya kiongozi wa mashtaka Bw Taib Ali Taib na Dkt Khaminwa na Bw Nyamu.

Kiongozi wa mashtaka Taib Ali Taib (kulia) aliyepinga vikali kesi ya ufisadi ya Sonko ikiahirishwa na kushoto wakili Wilfred Nyamu (kushoto) akiomba korti isitishe kesi ya Sonko.Picha/RICHARD MUNGUTI

Bw Taib aliwakabili Mabw Khaminwa na Nyamu akidai wanamtisha hakimu na kuhujumu kusikizwa kwa kesi ya ufisadi dhidi ya Bw Sonko ya Sh10m.

“Mawakili hawa wanahujumu kesi hii. Wamewasilisha ombi baada ya nyingine na sasa wanamtaka hakimu akome kusikiza kesi hii. Hii ni hujuma tupu,”alisema Bw Taib.

Mawakili Khaminwa na Nyamu walimjibu kwa maneno mazito na sauti ya kuguruma kwamba “hawatakubali Sonko aendelee kunyanyaswa na afisi ya DPP.”

Kufuatia makabiliano hayo makali hakimu alisimama na kuondoka huku mawakili wa Sonko wakiendelea kuzugumza.

Bw Sonko alidai hakimu huyo anapendelea upande wa mashtaka na hana imani atapata haki kamwe. Awali Bw Ogoti alikuwa ametupilia mbali ombi la Sonko lakumtaka ajiondoe kwenye kesi hiyo.

Ripoti ya matokeo ya vipimo vya afya ya Mike Sonko iliyowasilishwa na madaktari wanne wa Hospitali Kuu ya Kenyatta. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Bw Ogoti alisema hakuna sababu maalum Sonko amewasilisha kumwezesha ang’atuke katika kesi hiyo.

Pia alitupilia mbali ombi la Sonko aahirishe kesi hiyo kwa siku 60 kuwezesha Dkt Khaminwa, Nyamu na Assa Nyakundi kupokea faili za kesi hiyo kutoka kwa mawakili Cecil Miller na George Kithi walioacha kumtetea.

Bw Ogoti aliamuru kesi iendelee kusikizwa Machi 15, 2021.

You can share this post!

Malala alia kuna wizi wa kura Matungu

Mlinzi wa Malala akamatwa kwa kufyatua risasi hewani