• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:55 AM
Tanzia: Mwanafunzi amuua mwenzake kutokana na mzozo wa mapenzi

Tanzia: Mwanafunzi amuua mwenzake kutokana na mzozo wa mapenzi

Na TITUS OMINDE

POLISI mjini Eldoret wanachunguza kisa ambapo mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Eldoret anadaiwa kumdunga kisu mpenzi wake hadi kumuua.

Mara baada ya kisa hicho, mshukiwa aliyejulikana kwa jina la Elikana Kiplagat Korir alijaribu kujitoa uhai kwa kujidunga kwa kisu kifuani.

Polisi wanashuku kuwa tukio hilo la Jumapili jioni lilichochewa na mzozo wa kimapenzi.

Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Soy Henry Zuma alisema mshukiwa ambaye alikuwa katika hali mbaya alikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi kwa matibabu.

Bw Zuma alisema kuwa mwenye nyumba ya kukodisha ambamo marehemu alikuwa akiishi ndiye alimkimbiza mshukiwa hospitalini baada ya kuvunja nyumba hiyo kufuatia mvutano uliokuwa ukitoka chumbani humo.

Akizungumza na wanahabari Bw Zuma alisema kisa hicho kilitokea katika nyumba ya kupangisha ya marehemu katika Kituo cha kibiashara cha Sogome kilicho karibu na Chuo hicho.

Mshukiwa alikimbizwa hospitalini akiwa katika hali mahututi.

“Ni bahati mbaya kwamba tumepoteza msichana mdogo sana kufuatia kile kinachoshukiwa kuwa mzozo wa kimapenzi. Mshukiwa ambaye alijaribu kujitoa uhai kwa kujidunga kwa kisu alikimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) kwa matibabu,” akasema Bw Zuma.

Polisi walipata kisu kilichokuwa na damu kutoka eneo la tukio.

Bw Zuma alisema uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini cha tukio hilo.

Aliongeza kuwa polisi bado hawajabaini ni nini wawili hao walikuwa wakisomea chuoni humo.

“Kwa kuwa hatuna habari ya kutosha kuhusu tukio hilo, bado hatujabaini wawili hao walikuwa wakisomea nini chuo kikuu.”

Mmoja wa majirani wa marehemu ambaye hakutaka kutajwa jina alisema wawili hao walikuwa wamejifungia ndani ya nyumba hiyo kwa takribani siku nne kabla ya tukio hilo.

“Korir alikuja hapa siku nne zilizopita na tangu wakati huo alijifungia pamoja na mpenzi wake ndani ya nyumba kwa takriban siku nne kabla ya mzozo ulioshuhudiwa Jumapili,” alisema.

Mwili wa marehemu umehamishiwa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya MTRH, huku uchunguzi zaidi ukianzishwa.

  • Tags

You can share this post!

Familia yahofia jamaa zao 11 waliangamia Shakahola

MAADHIMISHO: LEBA DEI 2023

T L