• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Familia yahofia jamaa zao 11 waliangamia Shakahola

Familia yahofia jamaa zao 11 waliangamia Shakahola

RUTH MBULA na WYCLIFFE NYABERI

HELLENA Nyamoita, 78, na mtoto wake wa nne, Frank Mose, wamefadhaika kufuatia kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki ya wafuasi wanaohusishwa na mhubiri tata Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International.

Wanaishi kwa uchungu nyumbani kwao katika kijiji cha Mogusii, eneobunge la Borabu, Kaunti ya Nyamira kwa sababu watu 11 wa familia yao wanashukiwa kujiunga na kanisa hilo la mafunzo ya itikadi kali miaka minne iliyopita.

Tangu waondoke nyumbani kwa miaka hiyo yote, hawajawahi kuwasiliana nao tena hadi habari za makaburi hayo zilipowafikia. Wana hao Richard Mose (aliyeondoka na mkewe na watoto wanne) na Joseph Ntabo (aliyeondoka na mkewe na watoto watatu) ni wa umri wa miaka ya arobaini.

Jamaa zao wa Nyamira wanashikilia huenda wakawa wahanga wa ibada ya Mackenzie ambapo waumini walidanganywa kufunga hadi kufa eti ndipo wamwone Masihi.

Japo mama Nyamoita na mwana huyo wake hawawezi kuthibitisha moja kwa moja iwapo wanafamilia wao ni miongoni mwa miili iliyofukuliwa, wana wasiwasi kuwa huenda jambo baya likatokea wakati upasuaji wa maiti hizo utaanza ili kuzitambulisha.

Familia ya Nyamoita inaamini kwamba ndugu zao waliandikishwa kujiunga na kanisa la Mackenzie na kwamba baadhi yao walikuwa na tabia za ajabu zinazoendana na wafuasi wa mhubiri huyo tatanishi, kuhusiana na tafsiri za maandiko na mdahalo kuhusu ni lini dunia itakapofika mwisho.

Huku umri ukizidi kumsonga ajuza huyo, hajui cha kufanya lakini anahisi rohoni mwake kuwa upasuaji huo utakapoanza, huenda miili ya watoto au wajukuu wake ikapatikana miongoni mwa iliyofukuliwa Shakahola.

“Nitaenda wapi na kuuficha uso wangu? Watoto wangu waliniambia kwamba walikuwa wakitokomea nyikani. Kumbe huyu Mackenzie ndiye jangwa walilomaanisha?” alijiuliza mama huyu aliyeonekana mdhaifu.

“Ninahisi huzuni kwamba watoto wangu ambao nilitumia kila senti niliyokuwa nayo kuwasomesha wamepotoshwa na dini hiyo na hakuna mahali wanasikika miaka minne tangu waelekee Kilifi,” akaongeza.

Kinachomuumiza kisaikolokia hata zaidi Bi Nyamoita ni ripoti kuwa baadhi ya miili inayofukuliwa Shakahola ni ya watu wa familia moja waliokuwa wakifukiwa makaburi mamoja.

Taifa Leo ilipomtembelea Mama Nyamoita juzi nyumbani kwake karibu na mpaka wa kaunti za Nyamira na Bomet, alikuwa ndani ya nyumba yake akitafakari ni wapi msaada ungetoka.

Alisema, “wanangu walipokuja hapa, waliniambia walikuwa wameokoka na wamemwona Yesu. Waliniambia pia nifuate mfano huo ili niweze kwenda mbinguni pamoja nao. Nikawajibu Mungu ninayemtumikia akitaka kunipeleka mbinguni atanijia hapa nilipo. Walikasirishwa na majibu yangu,” mkongwe huyo alisema huku akitokwa na machozi.

Mmoja wa binti za Richard hata hivyo alipinga kuhama kwao na kwa sababu hiyo, walikata uhusiano wao naye.

Kabla ya mahojiano, alisikika akiambia kikundi cha wanakijiji wengi wa rika lake kwamba alikuwa amemwachia Mungu hatima yake.

Frank Mose, mkazi wa Kijiji cha Mogusii, Borabu, Kaunti ya Nyamira wakati wa mahojiano. Picha / Ruth Mbula.

Marafiki walikuwa wamekuja kumfariji na kumpa tumaini la kuamini kwamba mambo yatakuwa sawa, lakini alibaki bila kusadiki.

Mwanawe mkubwa Bw Mose, ambaye sasa anaishi naye, alisimulia jinsi ndugu zake wawili walirudi nyumbani mwaka wa 2019 na kuwaambia kwamba wamepata kanisa, ambalo lilikuwa limewahakikishia tiketi ya moja kwa moja ya kwenda mbinguni bila kumngoja Kristo kwa muda usiojulikana.

“Walijaribu kunishawishi kuacha kanisa langu la Kiadventista na kujiunga nao katika ‘njia mpya’ iliyovumbuliwa ya kwenda mbinguni lakini nikawapuuzilia mbali,” alisema Bw Mose.

“Tulifikiri walikuwa wanatania tu. Lakini tulikuja kujua uzito wao baada ya wawili hao (Richard na Joseph) kuwatoa watoto wao wote shuleni kisha kuwafungia ndani ya nyumba zao wakisema kwamba walikuwa wakizingatia vipindi vya maombi wakiwa tayari kukutana na Kristo.”

Kulingana na Mose, nduguze waliuza mali yao yote yakiwemo mashamba ya mgao wao waliorithi kutoka kwa mababu zao kabla ya kuelekea Kilifi na pesa nyingi.

Bw Mose alifichua mtoto mkubwa wa Richard aliyemtaja kuwa Brian alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa nne aliyekuwa akisomea Mahusiano Mema kwa Umma katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro.

Lakini babake alipomshawishi kujiunga na kanisa fulani huko Malindi, aliacha chuo kikuu na kurarua vyeti vyake vyote vya elimu.

Mose alikumbuka kupokea jumbe nyingi za simu kutoka kwa mmoja wa kaka zake ambazo alisema zilikuwa na mashaka kiasi kwamba zilimtaka kushutumu kanisa lake la SDA na kujiunga nao katika dhehebu lisilojulikana huko Kilifi.

“Joseph alikuwa na matumaini sana kwamba angeweza kunivutia kwa urahisi katika kanisa lao lakini nilisimama imara. Kila nilipojaribu kuwapinga, walionekana kuhamaki. Mwanzoni waliniambia kwamba walikuwa wameanza uinjilisti katika baadhi ya mitaa jijini Nairobi na kwamba ilikuwa ni suala la muda tu kabla ya kuingia nyikani kukutana na Masihi. Kutokana na hulka zao, walikuwa na misimamo thabiti na kali kuhusu mafundisho ya Biblia,” Bw Mose, ambaye ni mwalimu alisema.

Jijini Nairobi, walipokuwa wakieneza injili, Bw Mose alidai kuwa Richard mara nyingi alikuwa akiwapigia simu wikendi na kuwaambia wasikilize kituo cha televisheni ambacho alitaka watu wa nyumbani waangalie kwa makini na kufuatilia mienendo ya mahubiri yanayopeperushwa huko.

Joseph alifanya kazi Nairobi katika kampuni ya maji huku Richard akifanya kazi katika kampuni inayotoa huduma za usafirishaji wa mizigo.

Mara baada ya familia ya Nyamoita kujua kinachoendelea huko Shakahola, walituma ndugu zao wanne kujaribu kuwatafuta lakini hadi sasa hawajawaona. Jamaa hao bado wamepiga kambi huko.

 

  • Tags

You can share this post!

Polisi wawili waliouawa Nithi walikuwa katika shughuli zao...

Tanzia: Mwanafunzi amuua mwenzake kutokana na mzozo wa...

T L