• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 2:55 PM
Thierry Neuville amwaga Sh257,000 milioni kusaidia ndovu na vifaru kulindwa

Thierry Neuville amwaga Sh257,000 milioni kusaidia ndovu na vifaru kulindwa

Na GEOFFREY ANENE

MATUNDA ya Safari Rally yaendelea kuingia baada ya dereva nyota Thierry Neuville kutangaza kusaidia shirika la kulinda wanyapori na mazingira la Sheldrick Wildlife Trust kwa Sh257,256 mnamo Juni 28.

Mbelgiji huyo, ambaye hakuweza kukamilisha Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally baada ya gari lake la Hyundai i20 kuharibika ikisalia mikondo minne mnamo Jumapili, ametangaza hayo kupitia mtandao wake wa Twitter.

“Nafurahia kufadhili shirika la Sheldrick Trust kwa Euro 2,000 baada ya WRC Safari Rally,” alitanguliza.

Dereva huyo, ambaye aligonga umri wa miaka 33 hapo Juni 16, aliongeza, “Nimeridhishwa sana na kupendezwa na kazi yao nzuri ya kulinda ndovu, vifaru na wanyamapori.”

Neuville alikuwa katika orodha ya madereva 58 walioshiriki Safari Rally ambayo ilikuwa inarejea kwenye WRC tangu mwaka 2002.

Aliongoza Safari Rally kwa muda mrefu tangu siku ya pili ya mashindano hayo mnamo Juni 25 kabla ya gari lake kuharibika “suspension” ya gurudumu la nyuma la pembeni kulia katika mkondo wa Loldia1 mapema Jumapili.

Mfaransa Sebastien Ogier aliibuka mshindi akifuatiwa na Mjapani Takamoto Katsuta wote wakiendesha magari ya Toyota Yaris. Raia wa Estonia, Ott Tanak alikamilisha orodha ya madereva watatu wa kwanza akiendesha Hyundai i20.

“Bado tuna motisha, lakini kwa bahati mbaya bado tunakosa bahati. Nina uhakika kuwa tutarejea mashindanoni tukiwa na nguvu zaidi na kufurahia mwisho wa msimu,” alihitimisha Neuville.

You can share this post!

Vipusa wa Arsenal wapata kocha mpya

Magavana 3 wa Pwani mbioni kujijengea jina