• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 4:39 PM
Uhuru ataja mbinu za kuvumisha Raila

Uhuru ataja mbinu za kuvumisha Raila

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta jana Ijumaa alitangaza azma yake ya kujitosa rasmi katika siasa kumsaidia kinara wa ODM, Bw Raila Odinga kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Rais Kenyatta aliyekuwa akizungumza alipokutana na wabunge na maseneta wa Jubilee katika Ikulu ya Nairobi, alisema kuwa chama hicho kitaunga mkono Bw Odinga ambaye alisema “ataendeleza miradi yetu tuliyoanzisha na kutuheshimu”.

Kiongozi huyo wa nchi, Ijumaa alionekana kutoa mwelekeo kwa wandani wake kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakimshutumu kwa kusalia kimya huku wenzao wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) wakiendelea kujijenga kisiasa.

Viongozi wa Jubilee wanatarajiwa kukutana Februari 25 na 26 katika jumba la KICC jijini Nairobi ambapo wajumbe wataidhinisha marekebisho ya katiba ya chama, bendera na nembo mpya ya chama.

Baada ya mkutano huo wa siku mbili, viongozi wa Jubilee wataongoza kampeni za muungano wa Azimio la Umoja kuhakikisha kuwa Bw Odinga anazoa kura nyingi katika eneo la Mlima Kenya, kwa mujibu wa mbunge wa Kieni Kanini Kega.

Wabunge wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto hawakupokea mwaliko wa kuhudhuria mkutano wa jana katika Ikulu.

“Katika miezi miwili ijayo, tutaandaa msururu wa mikutano katika eneo la Mlima Kenya ili tuwaeleze ni kwa nini Bw Odinga ndiye anayefaa kuwa mrithi wa Rais Kenyatta,” akasema Bw Kega ambaye alihudhuria mkutano huo wa Ikulu.

Sababu ya kusalia kimya

“Chama cha Jubilee kimekuwa kimya kwa sababu tumekuwa tukitumikia wananchi. Kwa sababu sasa ni msimu wa siasa acha sasa tujitose kwenye siasa,” Rais Kenyatta aliambia viongozi hao.

Rais Uhuru analenga kuunda vikundi mbalimbali katika eneo la Mlima Kenya ambavyo vitatwikwa jukumu la ‘kuhubiri injili’ ya Bw Odinga.

“Rais Kenyatta atakutana na viongozi wa kila kikundi kuwapa mwongozo kuhusu jinsi ya kushawishi wakazi wa Mlima Kenya kukumbatia Azimio la Umoja,” mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Ngunjiri Wambugu, aliambia Taifa Leo.

Rais Kenyatta pia anatarajiwa kufanya msururu wa mikutano ya kisiasa katika eneo la Mlima Kenya kuwaeleza wakazi wa eneo hilo sababu za kuamua kumkumbatia Bw Odinga na kuachana na Dkt Ruto.

Rais Kenyatta aliambia wabunge wa Jubilee kuwa atasalia kuwa kiongozi wa chama hicho tawala na yuko tayari kukiongoza kuafikia malengo yake ya kuwa sehemu ya serikali ijayo.

“Lengo kuu la Jubilee ni kuunga mkono mwaniaji wa urais ambaye tuna maono sawa atakeyetuheshimu na kutujali. Tutaunda serikali ijayo kama washirika ili miradi tuliyoanzisha miaka 10 iliyopita iendelezwe,” Rais Kenyatta alisema.

Katika mkutano huo wa Ikulu, Kiongozi wa Nchi alitangaza mipango ya ‘kukipamba’ chama cha Jubilee ili kuwavutia wakazi wa Mlima Kenya ambao wengi wao wanaonekana kupendelea chama cha UDA cha Naibu wa Rais.

Katika mkutano wa jana, pia ilifichuka kuwa chama cha ODM cha Bw Odinga huenda kikalazimika kuachia Jubilee kusimamisha wawaniaji katika maeneo mbalimbali ya nchi kama vile Nairobi na Pwani.

“Kwa kuwa hatuna mwaniaji wa urais, itabidi tusimamishe wawaniaji wengi wa ugavana, useneta, ubunge na udiwani katika angalau kaunti 33 nchini,” akasema Bw Ngunjiri.

Kulingana na duru, chama cha ODM tayari kimekubali kuachia Jubilee kiti cha ugavana wa Nairobi licha Bw Odinga kusisitiza kuwa kitasimamisha mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi.

Jubilee inapendekeza mfanyabiashara Richard Ngatia kuwa mwaniaji wake wa ugavana.

ODM itatoa naibu gavana huku washirika wengine wa Azimio la Umoja wakiachiwa nyadhifa za uwakilishi wa wanawake na useneta.

Viongozi wa Wiper chake Kalonzo Musyoka na Kanu inayoongozwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi wanatarajiwa kukutana Jumatano kuidhinisha vyama hivyo kujiunga na Azimio la Umoja

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Jumuiya ya Afrika Mashariki iimarishwe...

Middlebrough yadengua Man-United kwenye Kombe la FA kupitia...

T L