• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Ukambi: Wazazi wahimizwa wakumbatie chanjo

Ukambi: Wazazi wahimizwa wakumbatie chanjo

Na KENYA NEWS AGENCY

WAZAZI wametakiwa kupeleka watoto wao wa umri kati ya miezi tisa na 59 kudungwa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa ukambi katika vituo mbalimbali nchini.

Mwakilishi wa wizara ya Afya, Dkt Tabitha Oketch aliyekuwa akizungumza katika Kaunti ya Garissa, alisema chanjo hiyo ni salama wala haina madhara yoyote kwa afya ya watoto.

Serikali inalenga watoto zaidi ya milioni tatu kutoka kaunti 22 katika kampeni hiyo ya siku 10 iliyong’oa nanga mnamo Ijumaa.

Kaunti zinazolengwa ni Mandera, Wajir, Garissa, Baringo, Pokot Magharibi, Turkana, Kilifi, Tana River, Trans Nzoia, Elgeyo Marakwet, Busia, Homa Bay, Migori, Kisii, Kajiado, Nairobi, Bomet, Bungoma, Kakamega, Narok na Vihiga.

Kaunti hizo zilibainishwa kufuatia utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) lililobaini kuwa visa vya ukambi ni mahususi katika maeneo hayo.

“Iki kupunguza kasi ya maradhi hayo tunahitaji kuhakikisha kuwa watoto wanapewa chanjo hiyo,” akasema Bi Oketch.

Kaunti ya Garissa inalenga kutoa chanjo hiyo kwa watoto 165,000 kufikia Julai 4.

Katibu wa Kaunti ya Garissa, Abdi Sheikh alisema chanjo hiyo itasaidia pakubwa katika juhudi za kuangamiza ukambi katika kaunti hiyo ya ukanda wa Kaskazini Mashariki.

Sheikh aliwataka machifu, viongozi wa makanisa, walimu na viongozi wa kaunti hiyo kusaidia katika juhudi za kuhakikisha watoto wanaolengwa wanadungwa chanjo hiyo.

“Tunahitaji ushirikiano wa kila mtu kuhamasisha jamii kupeleka watoto wao kudungwa chanjo ya ukambi,” akasema Bw Sheikh.

Waziri wa Afya, Roble Nunow alielezea matumaini yake kuwa asilimia 95 ya watoto wanaolengwa katika Kaunti ya Garissa watapata chanjo hiyo.

You can share this post!

Kiunjuri aonya Rais asijiongeze muda

Uhuru awapuuza wanaotilia shaka utendakazi wake