• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Usipozuia handisheki kati ya Ruto na Raila wewe kwisha, Kahiga aambia Gachagua

Usipozuia handisheki kati ya Ruto na Raila wewe kwisha, Kahiga aambia Gachagua

Na FLORAH KOECH

GAVANA wa Nyeri Mutahi Kahiga amesema kuwa kazi kubwa ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, ni kuhakikisha Rais William Ruto hatakuwa na handisheki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Akipuuza wanaoshuku uhusiano wa Bw Gachagua na mkubwa wake umeingia baridi, Gavana Mutahi alisema viongozi hao wawili wanaendeleza ushirikiano wa muda mrefu wa jamii zao mbili ambao umedumu kwa muda mrefu.

Alisema kuwa Bw Gachagua ni macho ya Mlima Kenya katika serikali ya Kenya Kwanza ili Rais Ruto asishawishike na kukubali Bw Odinga katika serikali yake.

“Tulimpatia mtu jasiri, Gachagua, kuwa naibu wake. Unajua wazi kuwa Rais wetu ni mtu wa dini sana na anaweza kuamua kumleta kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwa madai kuwa hataki kukosa mbinguni kwa sababu ya kutotii matakwa yake. Ndiyo maana tuna naibu rais ili kuepusha mawazo kama hayo,” akasema Gavana wa Nyeri, alipohudhuria ibada katika Kanisa la African Inland Church (AIC) huko Kabarnet, Baringo ya Kati.

Alisema wale wanaofikiri uhusiano wa rais na naibu wake umeingia doa wanashuku kitu kisichokuwepo.

“Yeyote anayedai kuwa Rais na naibu wake wamekuwa maadui anatakiwa kubadili miwani yake kwa sababu anachokiona si kweli kwa sababu uhusiano wao unazidi wao wawili. Huu ni uhusiano kati ya jamii mbili na wao wawili ni ishara tu,” alisema Gavana.

Rais Ruto na naibu wake wameonekana kutofautiana hadharani kuhusu ugavi wa nyadhifa katika Serikali ya Kenya Kwanza, kiongozi wa nchi akieleza kuwa hakuna eneo linalopaswa kubaguliwa kwa mujibu wa lilivyopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Akizungumza huko Nyanza hivi majuzi, alisema Wakenya wanahitaji kuhudumiwa kwa usawa na atazunguka nchi nzima kuhakikisha hilo linafanyika.

Hata hivyo Bw Gachagua anasisitiza ni waliounga Kenya Kwanza wanaofaa kupatiwa kipaumbele katika uteuzi serikalini na miradi ya maendeleo.

Gavana Kahiga alisema ni wakati muafaka wa Wakenya kuelewa kwamba hawafai kuzungumza kuhusu watu binafsi bali jamii mbili ambazo zilikubaliana mchana peupe kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya Wakenya wote.

Aliongeza: “Ukweli wa mambo ni kwamba, uhusiano wao ni thabiti na wa kirafiki. Binafsi nimepata fursa ya kuongea na wote wawili na hakuna tatizo kati yao. Hebu kila mtu aelewe kwamba umoja wao unapita zaidi ya watu wawili,” alisema.

Bw Gachagua amedokeza kuwa anaunganisha eneo la Mlima Kenya ili kumwezesha Rais Ruto kushinda uchaguzi wa 2027 kwa kura nyingi.

Aliihakikishia nchi kuwa serikali ya Kenya Kwanza chini ya Rais Ruto iko shwari na hakuna tofauti za kisiasa kati ya uongozi wa juu, ambao alisema, unashauriana kuhusu masuala yote yanayohusu Serikali.

  • Tags

You can share this post!

Ugonjwa unaomfanya mtu kujikuna anapogusa maji

Polisi aliyeua mumewe kuzuiliwa kwa siku 14 uchunguzi...

T L