• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Polisi aliyeua mumewe kuzuiliwa kwa siku 14 uchunguzi kufanyika

Polisi aliyeua mumewe kuzuiliwa kwa siku 14 uchunguzi kufanyika

NA TITUIS OMINDE

AFISA wa Polisi kutoka Kitengo cha Askari Tawala (AP) anayeshukiwa kumuua mumewe Mjini Eldoret, kwa kumpiga risasi mara 12 atazuiliwa kwa siku 14 ili kuruhusu wapelelezi kukamilisha uchunguzi.

Afisa huyo anayehudumu katika Kitengo cha Ulinzi wa Majengo (CIPU), ambaye amekuwa akifanyakazi katika afisi ya Shirika la Kukadiria Ubora wa Viwango Bidhaa Nchini (KEB) anasemekana kumuua mumewe katika kimetajwa kama kuchochewa na mzozo wa kifamilia.

Koplo Lilian Biwot, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Dennis Mikoyan, Jumatatu Oktoba 16, 2023.

Kupitia hati ya kiapo, afisa mpelelezi Stephen Nzau kutoka kitengo cha Upelelezi wa Uhalifu na Jinai (DCI) Kaunti Ndogo ya Moiben, aliiomba mahakama imruhusu kumzuilia afisa huyo mwenye umri wa miaka 34 kwa siku 14 akisubiri uchunguzi wa mauaji ya mumewe Victor Kipchumba, 36 yaliyotokea usiku wa Oktoba 14.

Akiwasilisha ombi hilo, Bw Nzau aliambia mahakama kuwa mshukiwa alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Eldoret alfajiri ya Oktoba 15 ambapo aliripoti ya kumpiga risasi mumewe iliwasilishwa.

DCI huyo aliambia mahakama kuwa uchunguzi wa maiti bado haujafanyika, ikiwa ni pamoja na kuandikisha taarifa kutoka kwa mashahidi wakuu.

Vile vile afisa huyo aliiambia korti kuwa bunduki aina ya AK 47 inayodaiwa kutumika katika mauaji hayo, bado haijachukuliwa kufanyiwa uchunguzi pamoja na risasi na vifurushi vilivyotumika.

Wakati huohuo, afisa huyo aliambia mahakama kuwa maisha ya mshukiwa yamo hatarini iwapo ataachiliwa kutokana na hasira kutoka kwa wananchi.

“Iwapo mshukiwa ataachiliwa mara moja anaweza kuhatarisha uchunguzi wangu. Wananchi bado wana hasira na hivyo kutishia maisha yake iwapo ataachiliwa hivi karibuni, naomba mahakama hii iniruhusu kumzuilia kwa siku 14 katika kituo cha polisi cha Eldoret ili kuniwezesha kukamilisha uchunguzi,” Bw Nzau aliambia mahakama.

Mshukiwa hakupinga ombi hilo ambapo korti iliruhusu polisi kumzuilia katika kituo cha polisi cha Eldoret Central kwa siku 14.

Kesi hiyo itatajwa Novemba 2.

Wakati wa kukamatwa kwake, tukio hilo lilidaiwa kuwa lilitokana na ugomvi wa kifamilia baina ya afisa huyo na marehemu mume wake ambaye ni baba wa watoto wao wanne.

Kisa hicho kilitokea katika nyumba yao ya kukodisha katika mtaa wa Kimumu, kiungani mwa mji wa Eldoret Jumamosi usiku.

Inasemekana mshukiwa aliripoti kazini usiku, kabla ya kurejea nyumbani kwake ambapo alizozana na mumewe waliyeachana na kumuminia risasi 12.

  • Tags

You can share this post!

Usipozuia handisheki kati ya Ruto na Raila wewe kwisha,...

Gavana Ndeti abubujikwa na machozi kuona waathiriwa wa...

T L