• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
Ugonjwa unaomfanya mtu kujikuna anapogusa maji

Ugonjwa unaomfanya mtu kujikuna anapogusa maji

Na WANGU KANURI

MNAMO mwaka wa 2016, Walter Simiyu, 30, alianza kuhisi mwasho kila wakati alipogusa maji na haswa akioga. Bw Simiyu alikuwa akijikuna sana haswa mikononi, miguuni, mapajani, kifuani na tumboni kila baada ya kuoga huku akifikiria kuwa hali hii ilisababishwa na kuoga kwa maji baridi.

Hata hivyo, alikuja kugundua kuwa hata maji moto yalikuwa yakimwathiri na akalazimika kutafuta matibabu.

“Nilielezwa na daktari wa ngozi (dermatologist) kuwa ulikuwa mzio wa temprecha ya ghafla ya mwili,” anafafanua.

Bw Simiyu anasema kuwa alielezwa kuwa maji yoyote yale atakayotumia kuogea yatakuwa na athari hiyo pindi tu yagusapo ngozi yake kwa sababu ya kubadilika kwa temprecha.

“Sasa ninalazimika kuoga haraka sana kisha nivae nguo hata ingawa nitajikuna ingawa si sana,” anasema.

Hata ingawa hajaathiriwa na unyanyapaa, Bw Simiyu anaeleza kuwa kunao watu ambao humwogopa kwamba atawaambukiza ugonjwa huo.

“Kuna binti mmoja aliogopa sana kuupata ugonjwa huu baada ya kulala kwenye kitanda kimoja nami.”

Dkt Nancy Omwenga, mtalaamu wa ngozi katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki, anaeleza kuwa ugonjwa huu almaarufu Aquagenic pruritus (AP) humfanya mtu ajikune baada ya kugusa maji hata ingawa hatasababishiwa vidonda.

“Mgonjwa anaweza akajikuna pindi tu ayagusapo maji kwa dakika 15 hadi saa moja. Magonjwa ya ngozi kama ukurutu (eczema), na kansa ya figo inayoathiri tyubu zake (renal cell carcinoma) pia humfanya mtu kujikuna atokapo kuoga. Isitoshe, ugonjwa huu huweza ukarithiwa kifamilia,” anafafanua.

Aidha, Dkt Omwenga, anasema kuwa kuoga mara nyingi huwa kunatoa mafuta asilia ya ngozi na kuifanya ngozi ibaki kavu na yenye kuwasha.

“Hali hii huathiri jinsia za kike na kiume huku wagonjwa wengi wakiwa wanaume haswa walio na umri wa miaka 40. Hata hivyo, watoto na vijana pia huathiriwa pamoja na wazee,” anaongezea.

Isitoshe, Dkt Omwenga asema kuwa ingawa ugonjwa huu unasababishwa na maji baridi, maji vuguvugu na yaliyo moto, baadhi ya wagonjwa hupendelea maji vuguvugu kwa sababu hayadhuru ngozi yao sana na kusababisha mwasho.

Hali kadhalika, ugonjwa huu huathiri viungo vyote mwilini lakini watu wengi hulalamikia kuhisi mwasho kwenye miguu, mikono, kifua na mgongo.

“Hata hivyo, wagonjwa wa AP huwa hawaathiriwi kwenye viganja vya mikono, miguu na utando wa kamasi (mucus membrane) kwenye midomo, pua na masikio. Hii ina maana kuwa wanaweza kuyanywa maji na wasiathiriwe hata kidogo.”

Ili kukabiliana na ugonjwa huu, Dkt Omwenga anashauri dhidi ya kutotumia sabuni zenye madini ya salfa, parabeni, metali, mentholi inayotokana na mti wa mnanaa (mint), manukato na bidhaa zinazotengenezwa na pombe kwani zinafanya ngozi iwe kavu na iwashe.

“Bidhaa za kuosha nguo zenye harufu nzuri kwenye taulo na taulo zilizopakwa rangi (dyed towels) zinaweza kusababisha kuwashwa baada ya kuoga,” anaongezea.

Isitoshe, Dkt Omwenga anashauri dhidi ya kutumia vifaa vya kujisugua ambavyo vinakwaruza, kujipaka mafuta yasiyo na harufu angalau dakika tatu baada ya kuoga ili kufunika umajimaji ulio kwenye ngozi.

“Unaweza ukaongezea bikaboneti ya sodiamu kwenye maji ya kuoga kwa kufuata ushauri wa daktari wako kuhusu kiasi utakachoweka. Usioge zaidi ya mara moja kwa siku kwa sababu kuoga mara kwa mara kunafanya ngozi iwe kavu na ipoteze mafuta asili,” anasema.

Vile vile, mgonjwa wa AP hafai kutumia muda mwingi kwenye bafu na anapojipangusa hafai kujisugua bali kugusagusa viungo vilivyo na maji (tap drying).

Chumba ambacho anavalia nguo pia kinafaa kuwa na mashine inayoongeza unyevunyevu ili kupunguza uwezekano wa ngozi kukauka kwa haraka. Mgonjwa husika anafaa pia kuvaa nguo zilizoshonwa kwa pamba au zile zisizombana.

“Epuka kujikuna unapohisi mwasho kwani unapoanzia haja hiyo huongezeka,” Dkt Omwenga anasema.

Hata ingawa chanzo cha mwasho huu kwenye ngozi hakijabainika, watafiti wanasema kuwa ugonjwa huu huathiri jinsi mtu anavyoishi na hata anavyoshirikiana na wenzake.

Kwa kuwa hakuna tiba maalum inayoweza kuzuia mwasho huo, Dkt Omwenga anashauri wagonjwa wajipake mafuta ya watoto kabla ya kuoga ili kuipa ngozi yao kizuizi cha kinga.

“Matumizi ya dawa zitakazozuia kujikuna na ambazo hazimfanyi mtu kusinzia (non-sedating antihistamines), dawa za kutuliza maumivu na tiba ya miale ya ultraviolet (ultraviolet therapy) pia husaidia lakini mgonjwa anapaswa kumuona daktari kwanza kabla ya kuanza matibabu ya aina hii,” anaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Katibu Mkuu KNUT anusurika kifo kwenye ajali mbaya ya...

Usipozuia handisheki kati ya Ruto na Raila wewe kwisha,...

T L