• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Vibiritingoma waliovamia mitaani wafanya waume wengi kukwepa kanisa, Wahubiri walalamika

Vibiritingoma waliovamia mitaani wafanya waume wengi kukwepa kanisa, Wahubiri walalamika

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya viongozi wa makanisa yaliyo mjini Thika katika Kaunti ya Kiambu, wameibua malalamiko wakisema idadi ya wanaume wanaofika Kanisani inapungua kila Jumapili kwa sababu vibiritingoma huwateka.

Wamesema kwamba Jumapili wanawake hao huzidisha njama za kupata wateja na washirika wengi hujipata kwa lojing’i wakirushana roho badala ya kuwa Kanisani.

“Tunataka serikali ishughulike na kutuondolea hawa wanawake katika mitaa kuanzia saa kumi na moja alfajiri hadi saa moja jioni,” akasema Askofu Martin Mulwa wa Kanisa la Sacred Ghost Terbanacle.

Alisema kwamba ibada za awamu na ushirika wa jioni huchukua siku nzima hadi saa mbili usiku “na huo ndio wakati ambao tungetaka vibiritingoma wadhibitiwe”.

Askofu Moses Njihia ameambia Taifa Jumapili kwamba haja yake kubwa ni kuona kundi hilo la watu likiheshimu siku ya Jumapili ambayo kwa Wakristo ni mahususi kwa kutekeleza ibada.

“Ikiwa nao wale wa Seventh Day Adventist (SDA) watatoa malalamiko wakitaka hata Jumamosi iwe katika marufuku hayo, tutawaunga mkono,” akasema Askofu Njihia.

Alisema kwamba washirika hutegwa kwa kuwa wanajulikana huwa wana pesa za sadaka.

“Hali hii imechochewa na ukweli kwamba baadhi yao huingia Kanisani kwa lengo la kuunda mtandao wa kuchota washirika wetu wa kiume,” akadai.

Kasisi David Njeru wa Kanisa la Anglikana alisema kwamba “ukahaba ni kinyume na sheria”.

Alisema mjadala unfaa kuwa wa kumaliza ukahaba mitaani kwa siku zote.

“Hatufai kama Kanisa kujiingiza katika mjadala unaotuangazia kama tunaounga mkono ukahaba wa Jumatatu hadi Jumamosi na kuukemea Jumapili. Huo ni unafiki,” akasema.

Mshirikishi wa kundi hilo linalokemewa mjini humo Bi Cecilia Ngugi alisema kwamba “ukiona injili yako inakosa washirika, badilisha mbinu za kuhubiri”.

“Acha wadhibiti washirika wao. Wa kuchotwa huwa amejichota kwanza. Ukiona mtu mzima anaamua kwa hiari kuenda njia fulani huwa amefanya uteuzi wa moyoni. Sote tuko kwa soko la kusaka wafuasi kwa manufaa ya kibinafsi,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mhandisi ajeruhiwa baada ya gari kukanyaga kilipuzi katika...

Shule yapata darubini, vifaa vingine sayansi ikigeuzwa...

T L