• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Video zenye uchochezi wa kisiasa kufutwa mitandaoni

Video zenye uchochezi wa kisiasa kufutwa mitandaoni

Na Winnie Atieno

VIDEO za wanasiasa zenye kauli za uchochezi zitafutwa mitandaoni na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria, katika juhudi za kukabiliana na uhasama wakati huu ambapo kampeni za uchaguzi zinashika kasi nchini.

Mkurugenzi wa Bodi ya Filamu Nchini, Dkt Ezekiel Mutua, alisema hatua hiyo inalenga kuzzuia wananchi kuchochewa kufanya ghasia dhidi ya wale wenye misimamo tofauti kisiasa.

Alieleza kwamba Wizara ya Mawasiliano itadhibiti habari zinazosambazwa kupitia kwa mitandao ya kijamii, ili kufuta kabisa kanda za wanasiasa zitakazolenga kuchochea Wakenya.

“Wanasiasa hupenda kutamka maneno ya uchochezi wakati wa kampeni, ambayo huishia kupeperushwa mitandaoni. Tutakumbana na changamoto zaidi kuliko yaliyotupata 2007, ambapo vituo vya lugha za kiasili zililaumiwa kwa kutumiwa kuchochea vita,” akasema.

Mkurugenzi huyo alihoji kuwa kampeni zinafaa kuendeshwa kwa uadilifu pasipo matamshi ya uchochezi.

Alikuwa akizungumza jana alipofanya ziara mjini Mombasa, ambapo pia aliwataka wanahabari kuwa makini ili wanasiasa wachochezi wasieneze matamshi ya kugawanya jamii kupitia taarifa zao.

 

You can share this post!

Ushuru wa miraa, muguka kupanda

Mamia wapoteza kazi UoN huku idara zikivunjwa