• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Ushuru wa miraa, muguka kupanda

Ushuru wa miraa, muguka kupanda

Na MAUREEN ONGALA

MADIWANI wa Kaunti ya Kilifi wamepitisha hoja ya kuitaka serikali ya gatuzi hilo kuongeze ushuru wa miraa na muguka.

Hoja hiyo iliyopendekezwa na Mwakilishi wa Wadi ya Garashi, Bw Peter Ziro, inanuia kufanya watafunaji miraa na muguka wapunguze uraibu huo.

Vilevile, inatarajiwa kuzidisha mapato ya serikali ya kaunti.Naibu Spika wa Kilifi, Bw Stanley Kenga, alisema madhara ya uraibu huo yanazidi kushuhudiwa katika jamii.

Hii ni pamoja na malalamishi ya wanawake kuwa waume zao wanapoteza muda katika utafunaji wa mimea hiyo, na kusahau majukumu ya ndoa.

Ni hivi majuzi tu ambapo wanawake walilalamika kupitia kwa shirika la kijamii la Kilifi Mums, kwamba waume wamewasahau kimahaba na kujitosa katika kutafuna muguka na miraa (almaarufu veve).

Pia wanafunzi wameripotiwa kutoroka shule ili kwenda ‘kuchana’ bidhaa hizo, huku vijana wakilazimika kuingilia uhalifu ili wapate pesa za kununua matawi na majani hayo mara kwa mara.Aliongeza kuwa kaunti pia inatarajia kuongeza mapato sheria hiyo mpya ikitekelezwa.

“Tunahitaji pesa zaidi kutumiwa kwa miradi ya maendeleo katika kaunti. Pia, naamini ushuru ukipandishwa wengi watajiepusha na utafunaji wa matawi haya ya kulevya, na hivyo athari zake zitapungua katika jamii,” akasema Bw Kenga.

Japo hoja hiyo iliungwa mkono na madiwani wengi ilipopitishwa, Diwani wa Mtepeni, Bw Victor Mwaganda, alionya kuwa huenda isilete manufaa yoyote.

Hii, alisema, ikizingatiwa kuwa kuna dawa zingine nyingi za kulevya ambazo ni ghali, lakini bado vijana huzitumia kwa wingi.

“Hatufai kufurahia pesa za miraa na muguka, ambazo zinamaliza vijana wetu. Tukiongeza ushuru ina maana kuwa waraibu watajitosa katika uhalifu ili wapate pesa za kununua vitu hivi,” alieleza.

Kwingineko, polisi wanawazuilia washukiwa watatu katika kijiji cha Jungu, Kaunti ya Kilifi, kwa madai ya kuwaua watu watatu.

Mshirikishi wa Kanda ya Pwani, Bw John Elungata, alisema jana kuwa maafisa pia wanawasaka watu wengine wanaodaiwa kuwahadaa waathiriwa hao watatu; wawili wa asili ya Asia na Mkenya mmoja, kabla ya kuwaua na kuteketeza gari lao.

“Washukiwa watatu tunaowazuilia wanahusika na mauaji hayo; tunaendelea kusaka wenzao,” alieleza.

Polisi wanaamini mauaji hayo yalitokana na mzozo wa shamba baina ya washukiwa na waathiriwa.

Kulikuwa na tetesi kwamba watatu hao waliuawa kwa sababu ya kushukiwa kuwa watekaji nyara ambao ni walanguzi wa viungo vya binadamu.

“Hatuwezi kutumia uvumi kwamba walikuwa walanguzi wa viungo vya mwili kuacha kusaka wauaji hao. Ni sharti waliotekelezwa kisa hicho wakamatwe na kufikishwa kortini,” akasema Bw Elungata.

Alionya raia dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao, na badala yake kuripoti washukiwa wowote wa uhalifu kwa chifu au kituo cha polisi.

Bw Elungata alisema mizozo ya ardhi katika eneo eneo hilo imekuwa ikichochea visa vya mauaji. Alitishia kuwachukulia hatua wanaoneza hofu kwa kudai kuwa waliouawa walikuwa watekaji nyara.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Korti zetu ziige mataifa mengine kuboresha...

Video zenye uchochezi wa kisiasa kufutwa mitandaoni