• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:08 PM
Mamia wapoteza kazi UoN huku idara zikivunjwa

Mamia wapoteza kazi UoN huku idara zikivunjwa

Na FAITH NYAMAI

MAMIA ya wafanyakazi wamepoteza kazi katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) huku serikali ikianza mchakato wa kufanya mageuzi katika mashirika ya serikali yanayopata hasara kulingana na mapendekezo ya Shirika la Kifedha la Kimataifa (IMF).

Baraza la UoN limepunguza idadi ya vitivo kutoka 35 hadi 11. Hiyo inamaanisha kuwa baadhi ya wafanyakazi katika vitivo vilivyoathiriwa wako katika hatari ya kupoteza kazi.

Hatua hiyo ilitokea siku moja baada ya Waziri wa Fedha Ukur Yatani Alhamisi kutoa orodha ya mashirika ambayo ni mzigo kwa serikali.

Bw Yatani alisema UoN, Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia (JKUAT) na Moi vimekuwa vikipata hasara hivyo vinahitaji mageuzi ili kupunguza gharama ya kuviendesha.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi, Prof Julia Ojiambo jana alisema nyadhifa tano za makamu wa manaibu chansela (DVCs) pia zimefutiliwa mbali.

“Kupunguzwa kwa vitivo mbalimbali na ofisi ambazo hutoa huduma sawa inaendana na maono ya chuo hiki,” akasema Prof Ojiambo.

Mwenyekiti wa baraza alisema taasisi 14 za utafiti, ikiwemo Taasisi ya Wangari Mathai (WMI) na Taasisi ya Masomo ya Maendeleo (IDS) zitaendelea kuhudumia jamii.Chuo Kikuu cha UoN kina jumla ya wafanyakazi 3,500; miongoni mwao waadhiri 1,500.

Prof Ojiambo alisema mabadiliko hayo yanalenga kupunguza gharama na kuondoa nyadhifa za maafisa wanaotekeleza majukumu sawa na wengine.

Naibu Chansela Profesa Stephen Kiama alisema mageuzi hayo yanalenga kurahisisha shughuli mbalimbali za elimu chuoni humo.

“Nyingi ya nyadhifa ambazo zimefutiliwa mbali zimekuwa kishikiliwa na watu ambao wamepewa kandarasi ya muda mfupi,” akasema Prof Kiama.

Naibu Chansela alisema mpango wa magezi hayo ulianza 2018.Kufikia sasa, wafanyakazi zaidi ya 100 wamepoteza ajira zao baada ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Nairobi kukataa kuongeza muda wa mikataba yao ya kazi.

Alhamisi, Bw Yatani aliorodhesha mashirika na taasisi za serikali ambazo zimekuwa zikipata hasara huku akisema zinahitaji mageuzi ya haraka kupunguza gharama ya kuziendesha.

Yatani alisema kuwa, baadhi ya taasisi na idara za serikali ni muhimu na zimekuwa zikihitaji kiasi kikubwa cha fedha kuziendesha hivyo kusababisha kuwepo kwa mrundiko wa madeni.

Mnamo Aprili, mwaka huu, shirika la IMF liliitaka Kenya kufanya mageuzi katika vyuo vikuu vitatu ili kuviokoa kutokana na mzigo wa madeni.IMF iliorodhesha Chuo Kikuu cha Kenyatta, UoN na Moi kama vyuo vikuu ambavyo viko katika hali ya hatari kifedha.

UoN kilitajwa kama chuo kikuu ambacho kimekuwa kikiendesha shughuli zake kwa madeni na kimeshindwa kulipa wafanyakazi wake pensheni, kulingana na ripoti iliyotolewa na Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA).

Vyuo vikuu vya umma vina jumla ya madeni ya Sh20.5 bilioni.Aprili, mwaka huu, IMF iliitaka Kenya kufanyia mageuzi mashirika na taasisi 18 ambazo zimekuwa zikipata hasara kabla ya kutoa mkopo wa Sh284 bilioni.

Mashirika mengine yanayolengwa katika mageuzi hayo ni Shirika la Ndege nchini (KQ), Shirika la Reli, Kenya Power, Shirika la Habari nchini (KBC), Baraza la Mtihani nchini (Knec) kati ya mengineyo.

You can share this post!

Video zenye uchochezi wa kisiasa kufutwa mitandaoni

Kalonzo, Kivutha waahidi kushirikiana katika maendeleo