• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:00 PM
Viongozi Uasin Gishu wasukuma Serikali iongeze bei ya mahindi wakitaja Sh4,000 kama dhihaka

Viongozi Uasin Gishu wasukuma Serikali iongeze bei ya mahindi wakitaja Sh4,000 kama dhihaka

NA STANLEY KIMUGE

SERIKALI ya Kitaifa inashinikizwa kuongeza bei ya mahindi ili kuwakinga wakulima dhidi ya gharama ya juu ya uzalishaji.

Viongozi wa Kaunti ya Uasin Gishu wanasema hawaelewi ni kwa nini mkulima anahangaika kuzalisha mahindi na pia kuhangaika kupata faida baada ya uzalishaji wenyewe.

Shinikizo hizi zinajiri wakati Serikali ya Kitaifa inapanga kununua vikaushio zaidi 100 ili kuzuia hasara ya baada ya mavuno huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha nchini.

Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi, alikuwa Uasin Gishu mnamo Jumanne ambapo Gavana Jonathan Bii na Seneta Jackson Mandago waliomba Serikali ya Kitaifa kufikiria kuongeza bei ya mahindi ili kuwaepusha na gharama ya juu ya uzalishaji.

“Hatuoni sababu ya mkulima kuhangaika kuzalisha mahindi na pia kuhangaika kupata faida baada ya uzalishaji. Tunataka kutoa wito kwa serikali kufikiria kuongeza bei au kuwapa wakulima motisha ya aina nyingine,” alisema Mandago.

Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) inatoa Sh4,000 kwa kila gunia la kilo 90 kwa sasa, huku serikali ikitenga Sh4 bilioni kwa ununuzi wa mahindi.

Lakini viongozi wa Uasin Gishu wanashinikiza bei ya Sh5,000 kwa kila gunia la kilo 90 ili kuwarahisishia wakulima wa mahindi mzigo wa gharama.

Uongozi wa kaunti pia unataka kupunguzwa kwa uzani wa gunia la mahindi kutoka kilo 90 hadi kilo 50 kama nafaka nyingine.

“Hatuoni ni kwa nini mahindi yanapimwa kwa kilo 90. Wizara ya Kilimo inafaa kupunguza uzani hadi kilo 50 kama vile vyakula vingine mfano wa mchele na viazi,” alisema Bw Bii.

Mbunge wa Soy, David Kiplagat, ambaye ni mwanachama wa kamati ya kilimo katika Bunge la Kitaifa alisema kamati hiyo imetenga Sh12.5 bilioni katika bajeti kuwezesha wizara hiyo kupata mbolea ya bei nafuu msimu ujao wa upanzi.

Bw Linturi alisema utawala wa Kenya Kwanza una nia ya kusaidia wakulima kupunguza hasara kwenye mashamba na kuhakikisha nchi inapata utoshelevu wa chakula.

Alisema kuwa tayari serikali imenunua vikaushio vya nafaka 100 kwa gharama ya Sh2 bilioni katika awamu ya kwanza ili kukabiliana na hasara ya baada ya mavuno katika kaunti 15 zinazokuza mahindi ambazo ni; Trans Nzoia, Uasin Gishu, Nakuru, Elgeyo Marakwet, Nandi, Bungoma, Kakamega, Poko Magharibi, Narok, Kericho, Migori, Bomet, Baringo, Nyandarua na Laikipia.

  • Tags

You can share this post!

Kalameni akemea ex wake kwa kumwandama warudiane

Pasta atuzwa runinga na LG/SJAK kwa ushabiki wakati wa Iten...

T L