• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Viongozi wataka Jaji Mkuu mpya ateuliwe kwa uwazi

Viongozi wataka Jaji Mkuu mpya ateuliwe kwa uwazi

Na SHABAN MAKOKHA

VIONGOZI kadhaa jana walijitokeza kuonya dhidi ya kuingiliwa kwa mchakato wa kumteua Jaji Mkuu mpya atakayemrithi David Maraga.

Wakiongozwa na Kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, walisema Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) yafaa kuachwa kuendesha shughuli ya kumsaka Jaji Mkuu mpya bila ya kuingiliwa na wanasiasa.

Akizungumza eneo la Khwiseri, Kakamega kwenye mazishi ya Dinah Isendi Muchelule, alisema idara ya Mahakama ni muhimu kwa ustawi wa nchi, na haifai kusimamiwa na mtu atakayekuwa kikaragosi cha wanasiasa.

Bi Isendi aliyezikwa kijijini Emalindi, wadi ya Kisa Mashariki, ni mamake Jaji Aggrey Muchelule. Idara ya Mahakama iliwakilishwa na Kaimu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu.

Gavana wa Kakamega Bw Wycliffe Oparanya alisema Idara ya Mahakama imekuwa ikitetea ugatuzi.

“Ni kutokana na kutetea ugatuzi baraza la magavana tulimwandalia karamu Jaji Mkuu aliyestaafu David Maraga. Tunawasihi majaji na mahakimu waendelee kutetea ugatuzi,” alisema Bw Oparanya.

Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, Bw Mudavadi aliwashauri Wakenya kumchagua kiongozi mwenye maono.

“Litakuwa jambo baya kwa Wakenya kuendelea kuwashangilia katika mikutano ya kisiasa viongozi wasio na maadili badala ya kuhoji ubora wao na sera zao kuhusu ufufuzi wa uchumi wa nchi hii,” alisema Bw Mudavadi.

Alisema Kenya kwa sasa inakabiliwa na wakati mgumu kiuchumi kwa vile wapiga kura walipotoshwa na kubebwa na mawimbi ya propaganda za viongozi wabinafsi na wanaojitikia makuu.

“Katika muda wa mwaka mmoja unusu uliosalia, Wakenya yafaa waache mchezo wa kamari wa kuwashabikia viongozi wasio na chochote cha manufaa kwa nchi hii. Najitolea mnichague kwa vile naweza kuvurumisha ufufuzi wa uchumi wa nchi hii na kuifanya nchi hii kuwa mahala bora pa kuekeza,” alisema Bw Mudavadi.

Katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (Cotu) Francis Atwoli alipuuza suala la kutokuwa na umoja wa jamii ya Waluhya akisema ni uzushi wa maadui wa Jamii ya Mulembe na wanahabari.

“Waluhya wako na umoja kama jamii nyingine Kenya. Katika maeneo yote, viongozi wanang’ang’ania uongozi. Katika eneo la Rift Valley Seneta Gedion Moi anamenyana na Naibu wa Rais Dkt William Ruto kuhusu ubambe wa eneo hilo huku jimbo la Ukambani Kalonzo Musyoka anatwangana na wanasiasa Johnstone Muthama, Kivutha Kibwana na Charity Ngilu wanaotaka uongozi pia. Hakuna mtu amesema hawana umoja,” alisema Bw Atwoli.

You can share this post!

Mikakati ya UhuRaila kutuliza mlima

DINI: Unapotubu na kuungama, Mungu mwenye rehema atakufuta...