• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:20 PM
Vita vya Obado dhidi ya Raila, ODM vingalipo

Vita vya Obado dhidi ya Raila, ODM vingalipo

Na IAN BYRON

GAVANA wa Migori Okoth Obado ameendelea kukishutumu chama cha ODM kwa kudai kilimtenga alipokabiliwa na changamoto katika muhula wake wa pili uongozini.

Obado anakabiliwa na kesi ya ufisadi ambapo amedaiwa kuiba Sh73 milioni pesa za umma katika serikali ya Kaunti ya Migori.

Mwaka 2020 ODM ilijaribu kumwondoa mamlakani kwa kudhamini hoja dhidi yake lakini njama hiyo iligonga mwamba.

Jumanne, Gavana huyo alitaja suala hilo kama mojawapo ya sababu zilizochangia uamuzi wake wa kugura ODM na kukumbatia chama cha Peoples Democratic Movement (PDP) kinachopania kushirikiana na chama cha United Democratic Movement (UDA) kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiongea na wakazi katika Wadi ya Wasimbete, kaunti ndogo ya Suna Magharibi, Jumanne, Obado alisema aliamua kufuata mkondo pinzani kisiasa kwa kudhulumiwa kila mara na vigogo wa ODM, chama kinachoongozwa na Raila Odinga.

Obado alidai viongozi hao wa ODM ndio walichochea masaibu yaliyomkumba katika muhula wake wa pili, baada ya kumshawishi kugura PDP iliyompa ushindi katika muhula wake wa kwanza 2013.

“Watu wangu, hawa watu walinihadaa nirejee katika ODM lakini kumbe walikuwa wakipanga kuniweka pabaya. Waliamua kunirusha ndani ya moto na ndio maana nimeamua kujiondoa na kupanga upya mustakabali wangu kisiasa ndani ya PDP,” akasema alipoongoza shughuli ya kuzindua ukarabati wa bwawa la Giribe.

Gavana huyo ambaye alikuwa ameandamana na Katibu wa Kaunti ya Migori Christopher Rusana na maafisa wengine, aliwasihi wakazi wa Migori kutowapigia kura viongozi wa ODM ambao wamekuwa wakimhujumu kisiasa tangu alipoingia mamlakani.

“Sitaki kushiriki vita vya ubabe na chama cha ODM. Lengo langu kuu ni kuvumisha chama mbadala ambacho kitachangia maendeleo katika eneo hili. Kupitia kauli yetu mbiui ya ‘Mamlaka kwa Wananchi’ nawahimiza msiwachague viongozi hao ambao hawakunipa nafasi ya kutimiza ahadi zangu kwenu,” Obado akasema.

Gavana Obado amekuwa akizozana na viongozi wa ODM katika Kaunti ya Migori na ngazi ya kitaifa kufuatia hatua yake ya kuhamia chama cha PDP mapema mwaka huu.Kwa upande wake, Bw Odinga amelaani hatua hiyo akidai gavana huyo anatumiwa na Naibu Rais William Ruto kudhoofisha ushawishi wake katika eneo pana la Nyanza Kusini.

Akiwahutubia waombolezaji katika hafla ya mazishi katika eneobunge la Nyatike Januari 23, 2021, Odinga aliongeza kuwa Bw Obado anaendesha njama ya kuleta migawanyiko miongoni mwa viongozi wa Nyanza kwa manufaa ya Dkt Ruto.

“Nilimwona Obado akisambaza wilbaro maeneo fulani hapa Migori. Nawaomba mkatae vifaa hivyo kwa sababu lengo lake ni kuwagawanya kwa manufaa ya yule adui wetu,” Bw Odinga akasema akiremrejelea Naibu Rais.

Wilbaro ni nembo ya chama cha UDA kinachohusishwa na Dkt Ruto na ambacho kinajaribu kukita mizizi yake eneo hilo kupitia ushirikiano wake na PDP.Bw Obado amekuwa akiendeleza ukaidi wake kwa ODM huku akiendelea kukivumisha chama cha PDP.

Ametangaza kuwa chama hicho kitadhamini wagombeaji katika uchaguzi mkuu ujao.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

  • Tags

You can share this post!

Wakazi Naromoru wahimizwa kuzingatia sheria na mikakati ya...

Wales wazamisha chombo cha Uturuki kwa ushindi wa 2-0...