• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:50 AM
Wakazi Naromoru wahimizwa kuzingatia sheria na mikakati ya kuzuia Covid-19 harusini na mazishini

Wakazi Naromoru wahimizwa kuzingatia sheria na mikakati ya kuzuia Covid-19 harusini na mazishini

Na SAMMY WAWERU

NAIBU wa Chifu kata ndogo ya Naromoru, Nyeri, Nyambura Githinji amewataka wakazi wa eneo hilo kwa jumla kuhakikisha wanazingatia sheria na mikakati ya Wizara ya Afya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Bi Nyambura amelalamikia baadhi ya hafla za umma kuandaliwa na washirika kukosa kutilia maanani mikakati kudhibiti kuenea kwa Covid-19.

“Nitazidi kukumbusha wakazi wa Naromoru kuzingatia sheria na mikakati ya wizara ili tusijipate katika hali inayoshuhudiwa katika baadhi ya mataifa,” akasema afisa huyo wa serikali.

Alisema hayo jana katika hafla ya maziko ya mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kabendera, Naromoru, mwendazake Immaculate Nyambura.

Marehemu Immaculate aliaga dunia siku kadha zilizopita, wakati akiendelea kupata huduma za matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi, baada ya kuugua kwa muda mfupi.

“Tunapohudhuria hafla za harusi, mazishi au mikutano mingineyo ya dharura ya umma, hakikisha aliyeketi karibu nawe yuko umbali wa zaidi ya mita moja na nusu na amevalia barakoa. La sivyo tutakuwa tukihatarisha maisha yetu sisi wenyewe, na mikusanyiko ya aina hiyo kupigwa marufuku,” Bi Nyambura akaonya.

Mazishi ya Immaculate yaliendeshwa chini ya saa tatu na kuzingatia vigezo vya kuzuia virusi vya corona, ambapo kila mwombolezaji aliyeingia alitakiwa kuwa na maski, na kutakaswa mikono kwa jeli.

“Maandiko ya Mungu yanatufunza kuwa watiifu, hivyo basi ni muhimu tuheshimu kanuni zilizowekwa kusaidia kuzuia msambao wa Covid-19,” akasema Askofu Njoroge Kahwai, msimamizi wa makanisa ya PEFA Kaunti ya Nairobi, na ambaye aliongoza mazishi hayo.

Askofu Njoroge Kahwai akihubiri katika hafla ya mazishi ya mmoja wa wakazi kijiji cha Kabendera, Naromoru, Kaunti ya Nyeri, ambapo alihimiza wenyeji kutii sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia kuenea kwa Covid-19. Picha/ Sammy Waweru

Himizo la viongozi hao limejuri wakati ambapo eneo la Nyanza na Magharibi mwa Kenya, amri ya ama kuingia au kutoka inanukia kuwekwa kutokana na kuendelea kusambaa kwa kasi kwa mfumbojeni wa virusi kutoka India.

Aina hiyo ya virusi ilitambuliwa humo mwezi wa Mei, na visa vya maambukizi vimepanda kwa kiwango kikubwa.

You can share this post!

Nina kiu ya kunolewa na kocha Ronald Koeman – Memphis...

Vita vya Obado dhidi ya Raila, ODM vingalipo