• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Wabunge wa Azimio wataka Chebukati, Guliye, Molu wachunguzwe kuhusu ubadhirifu wa raslimali

Wabunge wa Azimio wataka Chebukati, Guliye, Molu wachunguzwe kuhusu ubadhirifu wa raslimali

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Azimio la Umoja-One Kenya sasa wanapendekeza kubuniwa kwa Kamati Teule ya Bunge ili ichunguze mienendo ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati na makamishna wenzake wawili kubaini jinsi “wanavyotumia vibaya raslimali za umma na mamlaka ya afisi zao.”

Wabunge hao wa upinzani pia wanamtaka Bw Chebukati na makamishna Boya Molu na Abdi Guliye kuanza mchakato wa kuondoka afisini kuelekea kukamilika kwa muhula wao wa kuhudumu mnamo Januari 17, 2023.

Wakiongozwa na kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi wabunge hao wanawataka watatu hao kukoma kuendelea kufanya kazi na waelekee likizo wakijiandaa kustaafu.

“Maamuzi yote ambayo yalifikiwa bila kuhusisha makamishna wote, yakiwemo yale yanayohusu uchapishaji wa karatasi za kupigia kura katika uchaguzi mdogo na hatua ya Bw Chebukati kuwapandisha vyeo wafanyakazi yanafaa kubatilishwa,” wabunge hao wakawaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Jumanne, Novemba 22, 2022.

Bw Wandayi alikuwa ameandamana na wabunge; Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), Nabii Nabwera (Lugari), Tindi Mwale (Butere), Antony Oluoch (Mathare), miongoni mwa wengine.

Matakwa haya mapya ya wabunge wa upinzani yanajiri muda mfupi kabla ya mchakato wa kuondolewa afisini kwa makamishna wanne waliopinga ushindi wa Rais William Ruto, kuanza mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Katiba.

Wabunge wa Azimio pia wanataka Afisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu kufanya ukaguzi kuhusu matumizi ya fedha, haswa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Aidha, wanataka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya maafisa wa IEBC watakaopatikana na hatia ya ubadhirifu wa pesa za umma.

Wabunge hao wa Azimio walimsuta Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Hussein Marjan kwa kuvunja sheria kwa kuchapisha karatasi za kupigia kura kwa ajili ya chaguzi ndogo, ambazo zimeratibiwa kufanyika Desemba 8, 2022 na Januari 5, 2023.

“Kampuni ya Ugiriki ambayo ilichapisha karatasi za kura za kutumika katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ndio imepewa zabuni nyingine ya kuchapisha karatasi za kutumika katika chaguzi ndogo zijazo. Shughuli imefanywa bila kuhusishwa kwa makamishna wa IEBC, inavyohitajika kisheria. IEBC pia ilifaa kuchapisha karatasi hizo humu nchini kwa gharama ya chini,” akasema Bw Wandayi, ambaye ni Mbunge wa Ugunja.

Kiongozi huyo wa wachache alisema hakuna maelezo yametolewa kuelezea sababu iliyopelekea Bw Marjan, kuamua kivyake kutoa kandarasi ya uchapishaji karatasi za chaguzi ndogo.

Wabunge hao pia walipendekeza kuwa kupandishwa vyeo kwa wafanyakazi kulikofanywa na Bw Chebukati, bila kufanya mashauriano na makamshna wengine, kunafaa kufutiliwa mbali.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Pigo zaidi kwa Ufaransa baada ya...

Bidhaa zilizoundwa kwa maganda ya miwa, magazeti na vitabu...

T L