• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:31 PM
Waiguru aitaka Hazina ya Kitaifa kutoa fedha za Mei na Juni pia

Waiguru aitaka Hazina ya Kitaifa kutoa fedha za Mei na Juni pia

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru ameshabikia taarifa kutoka Waziri wa Fedha Ukur Yatani kwamba Hazina ya Kitaifa imetoa Sh43.5 bilioni kwa serikali za kaunti.

Akiongea na wanahabari jijini Nairobi Jumatano baada ya kufika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma (CPAIC), Bi Waiguru hata hivyo alisema fedha hizo ambazo ni za mwezi wa Aprili hazitasuluhisha changamoto zote za kifedha zinazozikabili kaunti.

“Napongeza Hazina ya Kitaifa kwa kutoa Sh43.5 bilioni za mwezi Aprili katika mwaka huu wa kifedha wa 2021/2022. Lakini ilipaswa kutoa pesa zote Sh107 bilioni ambazo zitajumuisha mgao wa mwezi wa Mei na Juni. Hii ni kwa sababu tunahitaji kuwalipa wadeni wetu ambao hutupa huduma kwa mkopo,” akasema Bi Waiguru.

Gavana huyo wa Kirianyaga vile vile, alipendekeza kuwa Hazina ya Kitaifa inafaa kuruhusu Serikali za Kaunti kuchukua pesa zinazolingana na mgao wao kisha kutoka kwa benki maarufu kwa kimombo kama “Banki Overdraft” endapo itachelewa kutoa fedha za mgao wa bajeti.

“Hili ni wazo zuri ambalo wiki jana lilitolewa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti. Endapo Hazina ya Kitaifa inafahamu kwammba itachelewesha fedha za kaunti, basi tuhuruhiwe kuchukua mkopo kutoka benki ili tuweze kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kisha ilipe pesa hizo baadaye,” Bw Waiguru akasema.

Katika taarifa yake, Waziri Yatani alisema pesa hizo zitapiga jeki shughuli za utoaji huduma katika kaunti hizo ikiwa ni pamoja na ulipaji madeni  inazodaiwa na wanakandarasi pamoja na wafanyabiashara walioziwasilishia bidhaa kwa mkopo.

“Ulipaji wa madeni utafuatiliwa kwa makini. Pesa zaidi zitatolewa kwa serikali za kaunti kwa misingi ya jinsi zilivyotekeleza wajibu huu muhimu kwa sekta ya kibinafsi,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Ana maono ya kucheza soka ya kulipwa

Droo ya Cecafa U23 kufanywa kupitia Zoom mnamo Ijumaa