• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wakazi 2,000 wa Kabati wafurika shuleni Mukerenju kwa matibabu ya bure

Wakazi 2,000 wa Kabati wafurika shuleni Mukerenju kwa matibabu ya bure

NA LAWRENCE ONGARO

ZAIDI ya wakazi 2,000 wa Kabati katika Kaunti ya Murang’a walinufaika na matibabu ya bure kupitia mpango uliosimamiwa na kampuni ya Delmonte.

Mkurugenzi wa kampuni ya Delmonte, Wayne Cook, alisema wameungana na wadau wengine ili kufanikisha shughuli hiyo muhimu.

Alisema saratani na maradhi mengine yamekuwa changamoto kwa watu wengi nchini.

“Tunaelewa ya kwamba kwa muda mrefu maradhi ya saratani yamekuwa tishio kubwa kwa watu wengi na kwa hivyo ni jukumu letu kuungana pamoja ili kukabiliana nayo,” alisema Bw Cook.

Wenyeji wa Kabati walifurika katika Shule ya Msingi ya Mukerenju ili kupata matibabu ya bure.

Wengi walikuwa na matatizo ya kisukari, damu kuchemka, matatizo ya macho, matatizo ya mifupa na maradhi ya tumbo. Pia walipimwa kubaini ikiwa walikuwa wanakabiliwa na aina yoyote ya saratani.

Wakongwe na watoto ndio walikuwa wengi wakati wa matibabu hayo.

Meneja mkuu wa maslahi ya wafanyakazi katika kampuni ya Delmonte Bw Gerald Matoke alisema ushirikiano wao na kampuni na watu wengine wenye maono sawa ni muhimu kwa mafanikio ya kiafya.

“Kampuni ya Delmonte itashirikiana kwa karibu na serikali kuu, serikali za kaunti za Murang’a na Kiambu, na washika dau wengine ili kuendeleza mipango ya upatikanaji wa afya kwa wote,” alisema meneja huyo.

Alisema kampuni ya Delmonte kila mara imekuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba inajali maslahi ya umma katika kaunti hizo mbili.

Mkurugenzi wa afya kaunti ya Murang’a Dkt James Mburu alisema kwa muda mrefu wamekuwa na ushirikiano wa karibu na kampuni ya Delmonte.

“Wagonjwa wengi wamepata matibabu kwa kukaguliwa na madakrari wenye ujuzi,” akasema Dkt Mburu.

Alieleza kuwa kuna haja ya kuwa na hospitali kadha mashinani ili kutosheleza matakwa ya wagonjwa wanaohitaji matibabu.

  • Tags

You can share this post!

Timu ya chesi ya KCB tayari kwa mashindano ya...

Wakusanyaji ushuru wasiofikisha pesa kwa ofisi kuandamwa...

T L