• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Wakazi 3,500 Mwatate hatarini kufurushwa

Wakazi 3,500 Mwatate hatarini kufurushwa

Na LUCY MKANYIKA

HATIMA ya wakazi zaidi ya 3,500 wa eneo la Mwatate, Kaunti ya Taita Taveta imo hatarini baada ya Shirika la Kuhufadhi Wanyamapori nchini (KWS) kutaka wafurushwe katika makao yao.

KWS imelalamika kuwa, wakati hao wamekataa kuruhusu ujenzi wa ua la stima katika hifadhi ya kibinafsi ya wanyamapori.

Kulingana na barua iliyoandikwa na msimamizi mkuu wa mbuga ya wanyama ya Tsavo, Bi Zainab Salim mnamo Mei 27, KWS inataka mbuga ya Taita Hills Wildlife Sanctuary iwafurushe maskwota katika sehemu ya ardhi ya Kamtonga-Alia.

Barua hiyo ilitumwa kwa msimamizi wa hoteli za Taita Hills and Saltlick.

Taharuki sasa imezuka katika eneo hilo baada ya wakazi kukataa kuhama kwa hiari katika ardhi ya ekari 2,000 ili kuwezesha ujenzi wa ua hilo la Sh40 milioni.

Mbuga hiyo ya kibinafsi inadai umiliki wa ardhi hiyo ambayo wakazi wanasema waliishi tangu miaka ya themanini. Ujenzi wa ua ulikwama kwa zaidi ya miaka kumi baada ya wakazi kuelekea mahakamani kuzuia KWS kutekeleza mpango huo wa ujenzi.

Baadaye mahakama iliagiza ujenzi wa ua katika sehemu ya Kamtonga-Alia uendelee.

Katika barua yake, Bi Salim alisema wakazi wanaoishi hapo wamechoma na kuiba vifaa vilivyonuiwa kutumiwa kwa ujenzi na kusababisha hasara.

Hata hivyo, wakazi wametaka serikali iharakishe kuwakabidhi hati miliki za ardhi hiyo badala ya kuwaacha wafurushwe.

Wakizungumza na Taifa Leo wikendi, walisema wakuu wa KWS na mbuga ya wanyama wanafaa kutatua tatizo la mizozo kati ya binadamu na wanyamapori eneo hilo badala ya kuzozania ardhi hiyo iliyo na madini.

“Sisi ndio wamiliki wa ardhi hii na hatutahama kutoka eneo hili,” akaapa mwenyekiti wa Chama cha Wakilima wa Alia, Bi Dorah Chao.

Kulingana naye, Mahakama Kuu iliagiza katika mwaka wa 1997 kwamba ardhi irudishiwe wenyeji.

Kupitia kwa baraza la wazee la Chawia, wakazi hao waliwasilisha ombi kwa bunge la taifa kusitisha ujenzi wa ua hadi mzozo kuhusu umiliki wa ardhi utatuliwe.

You can share this post!

Benteke atia saini mkataba mpya wa miaka miwili kambini mwa...

Dhuluma: Mbunge ahimiza wanawake wazungumze waziwazi badala...