• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Wakazi wa Kiambu wapatao 50,000 kupokea hatimiliki za ardhi

Wakazi wa Kiambu wapatao 50,000 kupokea hatimiliki za ardhi

NA LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Kiambu wapatao 50,000 wameahidiwa kwamba watapokea hatimiliki za mashamba yao katika kipindi cha siku chache zijazo.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro, alipongeza hatua ya rais Uhuru Kenyatta kuamuru wizara ya ardhi kuwapa wakenya milioni moja vyeti vyao vya mashamba.

Dkt Nyoro alisema wakazi wa maeneo tofauti kaunti ya Kiambu, watapokea vyeti vyao haraka iwezekanavyo ili waendelee kuishi kwa amani bila kutishwa na yeyote.

Baadhi ya maeneo yatakayonufaika na mpango huo ni Githurai na Ting’ang’a (vyeti vya ardhi 1000), Ndeiya – mjini Limuru – kutatolewa hatimiliki 25,000. Githunguri nayo itapokea vyeti 20,000.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi eneo la Gwa-Kairu Ruiru, alipofanya uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Gwa-Kairu-Kimbo-hadi Matangi, Juja, utakaogharimu takribani Sh20 milioni.

Ujenzi wa barabara ya Gwa-Kairu-Kimbo-hadi Matangi, Juja, unakadiriwa kwamba utakagharimu takribani Sh20 milioni. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alisema kwa muda mrefu wakazi wa Juja na Ruiru wameteseka sana na barabara mbovu huku biashara zao zikizorota.

“Ujenzi wa barabara hii ukikamilika nyinyi wakazi wa hapa mtanufaika pakubwa,” alifafanua gavana huyo.

Aliwarai wakazi kutoka maeneo kama vile Magharibi mwa nchi na kwingineko nchini waliojisajili katika eneo la Kati wapige kura bila kuwa na wasiwasi wowote.

“Serikali tayari imeweka mikakati ya usalama ambapo hakuna mtu yeyote atadhulumiwa na yeyote tunapoelekea kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022, ” alieleza Dkt Nyoro.

Aliwashauri wakazi wa Ruiru na Juja wawe makini wanapowachagua viongozi watakaowafanyia kazi.

“Kabla hujapiga kura yako fanya kuchunguza na ujiulize ni nini kiongozi amewatendea wakazi wa Ruiru na kwingineko. Huo ni msingi wa maisha yako ya baadaye,” alieleza gavana huyo.

Alisema kaunti itatenga takribani Sh1.3 bilioni za hazina ya Jiinue ili kunufaisha wanawake na vijana ili kuinua hali yao ya maisha. Aliwarai kujiweka kwa vikundi ili baada ya uchaguzi mwezi Septemba 2022, wapate fedha hizo.

  • Tags

You can share this post!

Mwamerika Fred Kerley afuta muda bora wa mita 100 alioweka...

Karata ya hesabu

T L