• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 6:50 AM
Wakazi wa Lamu wataka ahadi za Kibaki kwao zitimizwe

Wakazi wa Lamu wataka ahadi za Kibaki kwao zitimizwe

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Lamu wameitaka serikali kutimiza ahadi zilizotolewa kwao wakati wa ujenzi wa miradi iliyoanzishwa na utawala wa aliyekuwa rais Mwai Kibaki, kama njia mojawapo ya kumuenzi kiongozi huyo aliyeaga dunia.

Miongoni mwa ahadi hizo ni mpango wa kuwafadhili vijana 1,000 kimasomo na kuwalipa fidia wavuvi walioathirika na ujenzi wa bandari ya Lamu.

Rais huyo wa zamani ndiye aliyetangaza mpango wa serikali kuu kuwafadhili vijana wa Lamu kimasomo alipozuru eneo hilo mwaka 2012 kuweka jiwe la msingi la bandari ya Lamu.

Licha ya miaka mingi kupita na hata bandari ya Lamu kufunguliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta Mei 20, 2021, ni vijana 400 pekee ambao hadi sasa wameteuliwa na kufadhiliwa kimasomo huku hatima ya wengine 600 ikiwa haijulikani.

Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Mohamed Mbwana, alisema ipo haja ya vijana wote 600 waliosalia kuteuliwa kwa awamu moja na kufadhiliwa kimasomo. kama njia mojawapo ya kuheshimu kifo cha Rais Kibaki na azma yake kwa wakazi wa Lamu.

“Ni masikitiko kwamba Rais Kibaki amefariki wakati ndoto ya vijana 1,000 wa Lamu alionuia wafadhiliwe kimasomo na serikali kuu haijatimia,” akasema Bw Mbwana.

Mwanachama mwingine wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Muhashiam Famau, alisema kamwe hawamlaumu Kibaki kutokana na kufeli kwa serikali katika kutimiza ahadi hiyo.

Badala yake, Bw Famau aliwalaumu waliomrithi Kibaki kwa kuingiza siasa na kuchelewesha kutekelezwa kwa ahadi hiyo.Kulingana naye, mbali na ahadi ya masomo kwa vijana, wavuvi 4,734 wa Lamu hadi sasa wameishi kusubiri fidia ya Sh1.76 bilioni baada ya kuathiriwa na miradi ya kimaendeleo.

Anasema ili kuheshimu na kudumisha sifa njema ya Rais Kibaki, ni vyema serikali kuu na wasimamizi wa miradi hiyo iliyoanzishwa na Kibaki kuhakikisha matatizo yote ya kijamii yaliyotokea yanasuluhishwa kikamilifu.

“Tunamkumbuka Kibaki kwa kutuanzishia mradi mkuu wa bandari hapa Lamu. Pia tunakumbuka ahadi yake ya serikali kuu kutaka kufadhili vijana 1,000 wa Lamu. Tungeomba ahadi hii na pia fidia kwa wavuvi walioathiriwa zitatuliwe kwa heshima ya kifo cha rais wetu wa zamani, Mwai Kibaki,” akasema Bw Famau.

Kwa upande wake, Diwani wa Wadi ya Hongwe, Bw James Komu, alisema mbali na kuwafidia wavuvi na kufadhili vijana kimasomo, pia ipo haja ya serikali na wasimamizi wa bandari ya Lamu kuwapa vijana wa eneo hilo kipaumbele kiajira.

Bw Komu kadhalika aliwasihi viongozi wa sasa kuiga mwenendo wa Kibaki ambaye alithamini uongozi bora, hakuwa na majivuno wala malumbano na yeyote kinyume na hulka inayoonyeshwa na wanasiasa wa sasa.

“Tuige mwenendo mzuri wa Kibaki. Alikuwa mtaratibu, hakupenda mizozo wala ufisadi. Alithamini uchumi bora,” akasema Bw Komu.

  • Tags

You can share this post!

KASHESHE: ‘Chibu’ huyoo…azidi kupepea

IMF yashangilia huku Wakenya wakiongezwa ushuru wa bidhaa

T L