• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Wakili amshtaki Mbunge Salasya kwa kukataa kulipa deni la rafikiye   

Wakili amshtaki Mbunge Salasya kwa kukataa kulipa deni la rafikiye  

NA SHABAN MAKOKHA

WAKILI mmoja Kakamega amemshtaki Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, akimtaka kumfidia kwa kumshambulia kwa maneno.

Wakili huyo anadai Bw Salasya alimshambulia kwa maneno na kimwili kufuatia kesi ambayo mwanasheria huyo anashughulikia ambapo mbunge huyo anadaiwa kushindwa kulipa deni la Sh500, 000 alilokopa alipochaguliwa kuingia bungeni 2023.

Haya yanajiri baada ya mbunge huyo kutakiwa kufika mahakamani Novemba 8, 2023 kujitetea dhidi ya madai ya deni hilo ambapo mfanyabiashara, Robert Malenya Lutta alidai Salasya alishindwa kumlipa fedha hizo ndani ya miezi miwili kama walivyokubaliana.

Bw Edwin Wawire Wafula anaomba mahakama kuingilia kati, akidai mbunge huyo alimshambulia kwa maneno na kimwili mara mbili ndani ya mji wa Kakamega.

Mnamo Oktoba 30, 2023 Hakimu Mkazi Gladys Kiama alimtaka Bw Wafula, wakili wa Bw Lutta kumwasilishia Bw Salasya karatasi za mahakama kumwita afike kortini Novemba 8, 2023 wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo.

Lakini Novemba 2, 2023, mwendo wa saa kumi na mbili jioni, Bw Wafula anadai kuwa mbunge huyo alimshambulia kwa matusi na vitisho akiwa katika hoteli moja mjini Kakamega.

“Wafula wewe ni mtu mjinga sana. Utajua kuwa mimi ni mtu wa heshima. Niache vile ulivyoacha matiti ya mama yako. Wewe ni mdanganyifu – digrii yako ya sheria ni bandia. Nitakumaliza ikiwa hautaachilia kesi hiyo. Wewe ni mpumbavu na utanijua mimi ni nani,” Bw Wafula alisema hayo yalikuwa maneno aliyorushiwa na Bw Salasya kabla ya kufukuzwa na wasimamizi wa hoteli hiyo.

Tarehe hiyo hiyo, saa nane usiku, wawili hao walikutana tena katika kituo kingine cha Kakamega na mbunge huyo anasemekana kumshambulia kimwili wakili huyo.

Lakini alizuiliwa na kufukuzwa nje na wasimamizi wa Vault Hotel.

Wakili huyo aliripoti visa hivyo katika kituo cha polisi cha Kakamega kupitia nambari za matukio (OB Number) 02/11/2023/90.

“Maneno yaliyotamkwa na Bw Salasya hadharani, kwa maana yake ya asili, yananiashiria kama mtu mdanganyifu, mjinga, tapeli, mtu wa kishetani na mtu asiye na uadilifu. Kwa hivyo, nataka afafanue maneno haya mbele ya Mahakama kwa sababu hayakuwa tu ya kukashifu bali ni vitisho,” akasema Bw Wafula.

 

  • Tags

You can share this post!

Madereva 194 kupata kazi kaunti ya Nairobi ikijiandaa...

Kalonzo ampongeza Mdhibiti wa Bajeti kwa kufichua serikali...

T L