• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Kalonzo ampongeza Mdhibiti wa Bajeti kwa kufichua serikali hutenga pesa za kuendeleza ufisadi

Kalonzo ampongeza Mdhibiti wa Bajeti kwa kufichua serikali hutenga pesa za kuendeleza ufisadi

NA NDUBI MOTURI

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, ameilaumu serikali kutokana na kuongezeka ufisadi kwenye bajeti na kuanza utekelezaji wa vitambulisho vya kidijitali, licha ya hali ngumu ya kiuchumi ambayo nchi inapitia.

Bw Musyoka alisema utekelezaji wa mpango huo si muhimu kwa sasa, licha ya kupewa kipao mbele na serikali.

Kiongozi huyo alisema kuwa ufichuzi wa Msimamizi Mkuu wa Bajeti (COB) Margaret Nyakang’o, kwamba amekuwa akilipwa mshahara wake mara tatu zaidi ya kiwango kinachotakikana wakati nchi inapitia hali ngumu, ni ishara kwamba utawala wa Kenya Kwanza umepoteza mwelekeo.

“Msimamizi wa bajeti alifika mbele ya Kamati ya Mazungumzo ya Maridhiano na alizungumza kama mtaalamu. Tulimsikiliza kwa makini. Aliwasilisha takwimu, ambapo mambo aliyosema yalituacha katika mshangao. Alisema hakupata ufafanuzi kuhusu sababu ambapo mshahara wake ulizidishwa mara tatu huku, ukilipwa watu wengine, wala si yeye. Tunangoja maelezo kutoka kwa serikali,” akasema Bw Musyoka.

Alisema pia Wizara ya Fedha inafaa kujitokeza wazi na kutoa ufafanuzi kuhusu ufichuzi uliotolewa na Bi Nyakang’o kuhusu wizi wa fedha za umma.

Mazungumzo

Akirejelea mazungumzo ya maridhiano yanayoendelea na ambayo ripoti yake inatarajiwa kutolewa wiki chache zijazo, Bw Musyoka alisema kwa mrengo wa Azimio la Umoja bado unashikilia kuwa lazima kuwe na ukaguzi kuhusu uchaguzi wa urais mwaka 2022 na kushughulikiwa kwa gharama ya juu ya maisha.

Bw Musyoka alionya kwamba muungano huo utachukua hatua ikiwa masuala hayo mawili hayatashughulikiwa.

“Nawarai wabunge wasiisaliti nchi. Tunawahitaji watu waadilifu kama msimamizi wa bajeti. Kama Wakenya, msitamauke. Bado hatujapata suluhisho kuhusu yale yaliyofanyika kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2022. Wakenya wanapitia hali ngumu ya kimaisha, lakini serikali ishaanza kampeni za 2027. Tunaendelea na mazungumzo. Ikiwa hawatafanya tunavyowaagiza, mtaona,” akasema.

Vile vile, alimlaumu Rais William Ruto kuhusu mipango ya kuanzisha vitambulisho vya kidijitali, akiitaja kuwa kinyume na azma ya Wakenya wengi.

“Serikali imesema inataka kuanzisha vitambulisho vya kidijitali. Hiyo ni ishara kwamba nyakati za mwisho zimefika. Wahubiri na viongozi wa kidini wanafaa kujitokeza na kutueleza. Rais Ruto mwenyewe alisema watakuwa wakitumia macho yenu kuwatambua. Eti mtoto wako akizaliwa, atawekwa kidude. Tumekataa hayo,” akaongeza.

Bw Musyoka, aliyehudumu kama Makamu wa Rais kati ya 2008 na 2013, alikuwa akihutubu katika Kanisa la Kiadventista la Umoja II, Nairobi, ambapo alikuwa ameandamana na Maseneta na wabunge kutoka Azimio.

Wakati wa hafla hiyo, viongozi walisema kuwa gharama ya juu ya maisha ndilo suala linalofaa kupewa kipao mbele kwenye ripoti ya kamati ya mazungumzo ya maridhiano.

Walisema kuwa ikiwa hilo halitatimizwa, basi Wakenya wataanza kuandamana tena.

Viongozi kadhaa pia walimsifu Bw Musyoka kwa ushujaa wake, wakisema kuwa atakuwa debeni kwenye uchaguzi mkuu wa urais 2027.

  • Tags

You can share this post!

Wakili amshtaki Mbunge Salasya kwa kukataa kulipa deni la...

Mark Zuckerberg auguza jeraha la goti akijiandaa kushiriki...

T L