• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Wakulima wataka serikali iwape bima ikiwa El Nino itaharibu mazao yao

Wakulima wataka serikali iwape bima ikiwa El Nino itaharibu mazao yao

TOM MATOKE na EVANS JAOLA

Kenya inafaa kuanzisha kampuni ya bima ya kufidia wakulima wa mashamba madogo ambao huenda mimea yao ikaharibiwa na mvua ya Eli-Nino.

Wakulima wanasema kwamba serikali haijakuwa ikifidia wakulima mimea yao inapoharibiwa na viwavi jeshi na wakaongeza kuwa inafaa kuanzisha hazina spesheli kupitia kampuni ya bima ambayo itahakikisha wote watakaoathiriwa na El-Nino watafidiwa.

Wakulima hao walisikitika kwamba mojawapo ya sababu za Wakenya kuendelea kuteseka kutokana na uhaba wa chakula ni kuwa serikali haijaweka mfumo kuhakikisha wakulima wanafidiwa mimea yao inapoharibiwa kwa kuwa huwa wamewekeza pesa katika kilimo.

Wakulima hao wa mashamba madogo ya chai, mahindi na mifugo kutoka Nandi walieleza kuwa katika utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, wizara ya kilimo ilipanga kuanzisha kampuni ya bima kusaidia wakulima waweze kuimarisha utoshelevu wa chakula Kenya.

Wakiongozwa na mwenyekiti kiwanda chai cha Siret, Bw Wilson Tuwei Joseph Manjoy wakulima hao walisema kwamba katika nchi zilizoendelea, wakulima huwa wanafidiwa na serikali mimea yao ikiharibiwa na majanga na wakataka hatua sawa kutekelezwa Kenya.

“Kabla ya mvua ya El Nino, serikali inafaa kuchukua hatua na kuanzisha hazina spesheli ambayo itasaidia wakulima ambao wataseka mvua kubwa itakapoanza na mimea kuharibiwa kwa kuwa hii itaathiri mkulima,” alisema Tuwei.

Serikali ya Jubilee, kupitia wizara ya Kilimo ilikuwa imeahidi wakulima ambao mimea yao inaweza kuharibiwa na hima viwavi jeshi kuwa wangefidiwa lakini ahadi hiyo haikutimizwa.

“Wakulima ambao mimea yao iliharibiwa na viwavi jeshi sasa watafidiwa na serikali kupitia kampuni ya bima ambayo itaanzishwa na ambayo itashughulika na mimea ili Kenya iweze kuwa na utoshelevu wa chakula na kuhakikisha serikali itatekeleza kikamilifu ajenda zake,” aliyekuwa naibu waziri katika wizara ya kilimo wakati huo Dkt Andrew Tuirmur alisema.

Mamia ya hektari za mimea ya mahindi ziliharibiwa na uvamizi wa viwavi jeshi kote nchini mwaka wa 2018 na tayari serikali ilikuwa imetumia 350 milioni kuangamiza viwavi hao.

Haya yanajiri huku gavava wa Trans Nzoia George Natembeya akisema kaunti yake imejiandaa kukabiliana na athari za mvua ya Elnino. Hata hivyo aliwahimiza wakulima kuvuna mazao yao mapema kuzuia hasara baada ya mavuno.

Bw Natembeya alisema kwamba serikali yake itaanzisha kituo cha kushughulikia matukio ya dharura yatakayotokana na mvua ya El Nino.
“Tumeunda timu ya maafisa kutoka idara tofauti kutambua maeneo hatari kwa mafuriko na matukio mengine lakini tunahimiza wakulima kuvuna mazao yao mapema,” Bw Natembeya alisema.

Miongoni mwa mikakati ya kaunti hiyo ni kuwa na dawa za kutosha katika vituo vya afya kukabiliana na mkurupuko wa maradhi unaoweza kuzuka na kutoa misaada ya kibinadamu.

  • Tags

You can share this post!

Mazungumzo Bomas: Cotu yawafisha moyo waliolemewa na...

Wetang’ula awaonya wanaolemaza mazungumzo ya Bomas

T L