• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 9:55 AM
Wetang’ula awaonya wanaolemaza mazungumzo ya Bomas

Wetang’ula awaonya wanaolemaza mazungumzo ya Bomas

NA BENSON MATHEKA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amewataka wawakilishi katika mazungumzo ya pande mbili kujiepusha na tofauti zinazoweza kulemaza na kusambaratisha mazungumzo hayo.

Bw Wetang’ula alisema kwamba kuna wasi wasi kuhusu vita vya maneno kati ya wanachama wa Kenya Kwanza na Azimio katika mazungumzo ya Bomas of Kenya na akawataka wasipoteze mwelekeo.

“Nimeona wawakilishi wa mazungumzo ya pande mbili wakigombana. Nawaomba wasipoteze mwelekeo. Wawe makini na kuleta usawa ambao Rais alitamani nchi iwe nao,” alisema Spika.

Akizungumza katika shule ya upili ya wasichana ya Chwele eneo bunge la Sirisia, Kaunti ya Bungoma ambapo aliwaongoza zaidi ya wabunge 20 katika harambee ya kufadhili shule hiyo, Bw  Wetang’ula alisema kuwa mazungumzo hayo yaliidhinishwa Bungeni chini ya  uongozi wake  kama Spika na atayalinda dhidi ya yeyote anayetaka kuyasambaratisha.

Wetang’ula ambaye aliandamana na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kwa mara nyingine aliwataka viongozi katika eneo hilo kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuungana kwa ajili ya ustawi wa jamii.

“Wakati huu tunataka jamii zote za eneo la Magharibi kutembea pamoja. Mwelekeo wetu hauwezi  kufaulu bila jamii zote zinazoishi katika eneo hilo,” alisisitiza.

Kuhusu Mswada wa Sukari mbele ya Bunge la Kitaifa, Wetang’ula alibainisha kuwa alikuwa na matumaini kuwa utapata kibali kutoka kwa Wabunge.

“Nilikuwa Mombasa na kukutana na wenyeviti wote wa Kamati katika Bunge la Kitaifa kujadili Mswada huo. Ninataka kuwahakikishia wakulima kwamba utapewa kipaumbele na utafaulu,” akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Wakulima wataka serikali iwape bima ikiwa El Nino itaharibu...

Mshukiwa wa mauaji ya kikatili ya Afisa Mkuu wa Fedha...

T L