• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wanajiji walivyochana mbuga betri ya baiskeli ya umeme ilipolipuka

Wanajiji walivyochana mbuga betri ya baiskeli ya umeme ilipolipuka

NA WINNIE ONYANDO

MWENDO wa saa tatu unusu asubuhi siku ya Jumatano, Desemba 12,2023, mlipuko wa kutisha ulisikika katikati mwa jiji la Nairobi (CBD) ukifuatwa na wingu la moshi.

Wengi wakichukua gari nambari mguu niponye, walihofia huenda moto umetokea katika kitovu cha jiji la Nairobi.

Hata hivyo, Taifa Leo Dijitali ilipofika kwenye eneo la tukio, iligundua kuwa ni betri ya baiskeli inayotumia nguvu za umeme ndiyo ililipuka.

Mwathiriwa alieleza kwamba kisa hicho kilitokea muda mfupi tu baada ya kuchukua betri yake iliyokuwa ikipata chaji kwenye ghorofa moja jijini.

Alipokuwa akitoka nje, alijikwaa na kuanguka.

Betri hiyo ilipoanguka chini, ilianza kuvimba.

Kwa kutambua hatari inayoweza kusababishwa na kifaa hicho, mwathiriwa alikimbia na kuitupa nje ya jengo hilo ikaishia kulipuka.

Kutokana na tukio hilo, lazima tujiulize ikiwa betri ya baiskeli, bodaboda au gari linalotumia nguvu za umeme ni salama kwa matumizi?

Kulingana na tatafiti mbalimbali, kulipuka kwa betri za baiskeli ya umeme kunahusishwa na masuala kadha wa kadha, ikijumuisha vifaa mbovu vya kuchaji, mbinu zisizofaa za kuchaji, na soketi za umeme zilizojaa kupita kiasi.

Ingawa wengine wanapendelea mfumo wa kubadilishana betri, wengine wanaafadhalisha kuchaji betri na kusubiri hadi ijae.

Bei ya baiskeli za umeme ni kati ya Ksh100, 000 na Ksh300, 000.

Kisa hicho kinajiri huku mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ukikamilika Dubai.

Katika makubaliano ya Kongamano hilo la hali ya hewa, viongozi wa nchi mbalimbali walikubaliana kupunguza uzalishaji wa gesi hatari ya Kaboni jambo ambalo lilimfanya Rais William Ruto kukumbatia matumizi ya magari, baiskeli na bodaboda za umeme.

Septemba 3, 2023, Rais Ruto aliendesha gari dogo linalotumia nguvu za umeme, kuelekea katika Ukumbi wa KICC, Nairobi ambapo Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi Barani Afrika 2023 lilifanyika.

Rais alichukua hatua hiyo kuonyesha mpango wa serikali yake ya kupunguza uzalishaji wa Kaboni.

Kenya inakadiriwa kuzalisha asilimia 0.1 ya gesi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Familia yazika mgomba wa ndizi hospitali ikikataa na mwili

Wafanyabiashara wa ‘mahaba’ Kikopey walalamikia ukosefu...

T L