• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Wafanyabiashara wa ‘mahaba’ Kikopey walalamikia ukosefu wa maji

Wafanyabiashara wa ‘mahaba’ Kikopey walalamikia ukosefu wa maji

NA RICHARD MAOSI

WAHUDUMU wa biashara ya mahaba eneo la Kikopey, barabara ya Nakuru-Nairobi, wametishia kuongeza ada ya huduma wanazotoa kwa sababu ya kukatika kwa maji mara kwa mara.

Wanatafuta maji mbali, na yanayopatikana ni kutoka kwa wachuuzi, wakilalamika kwamba wanauziwa bei ghali mno.

Ni tatizo ambalo limefanya baadhi ya wateja wao kukosa maji ya kuoga na hivyo basi kutorokea miji jirani ya Nakuru, Naivasha, Salgaa, Mlolongo na Maai Mahiu.

“Tunaomba Shirika la Usambazaji maji na Udhibiti wa Majitaka Nakuru kutoa mgao sawa wa maji kwa watu wote.”

Hii ni kulingana na kiongozi wao ambaye tutamwita Dee maana hakutaka kunaswa na kamera zetu wakati wa mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali.

Kulingana na Dee, upatikanaji maji utafanya bei ya huduma kuwa nafuu.

Dee anasema baadhi ya wafanyabiashara wenza wameamua kujinyima kiasi kwamba wanahifadhi maji yanayopatikana kwa ajili ya wateja wao.

Anasema wateja wao wengi ni madereva wa malori ya masafa marefu, na kwamba huwa wamekita kambi Kikopey kujivinjari au kutuliza mawazo.

Jambo linalokera ni kwamba hulazimika kuwatoza ada ya ziada, ikiwa ni pamoja na kugharamia maji.

“Isitoshe wengi wetu tunaoga mara moja au mbili kwa wiki na wengine baada ya siku kadhaa kwa sababu ya bei ghali ya maji yanayochuuzwa hapa,” akasema.

Dee anasema punda waliokuwa wakitegemewa sana na wachuuzi kwa ajili ya kusafirisha maji kutoka miji jirani ya Gilgil wameanza kupungua.

Uhaba wa maji Kikopey unazidi kushuhudiwa hasa baada ya kuripotiwa visa vya punda kutoweka, changamoto inayotajwa kuchangiwa na biashara haramu ya uuzaji nyama za punda.

Ikumbukwe kuwa Kikopey ni eneo ambalo limekuwa likishuhudia idadi kubwa ya shughuli za kibiashara, uchuuzi na mikahawa inayofanya kazi saa 24 mfululizo.

Kwa miaka mingi, ukosefu wa maji umekuwa ukikumba maeneo mengi yanayozunguka Kaunti ya Nakuru haswa msimu wa kiangazi unapokaribia

Tunapokaribia msimu wa sherehe za mwisho wa mwaka, warembo kutoka Nyandarua, Kinangop, Narok, Kiambu na Machakos wamejaa Kikopey.

Wanalenga kujichumia riziki hasa wakati huu ambao biashara zao huwa zimenoga.

  • Tags

You can share this post!

Wanajiji walivyochana mbuga betri ya baiskeli ya umeme...

Wanasiasa Kisii wanaopepeta moto wa fujo kuona cha mtema...

T L