• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:26 PM
Wanasaikolojia wajadili ongezeko la visa vya watu kujitoa uhai

Wanasaikolojia wajadili ongezeko la visa vya watu kujitoa uhai

Na LAWRENCE ONGARO

WASHAURI wa maswala ya kisaikolojia wapatao 50 kutoka Kaunti ya Kiambu walijumuika pamoja mjini Thika ili kujadili matukio tofauti yanayoshuhudiwa ya watu kujitoa uhai katika siku za hivi karibuni.

Wataalam hao walisema wamegundua ya kwamba kwa siku za hivi karibuni watu wazima na hata vijana wamejitoa uhai kutokana na msongo wa mawazo.

Akizungimza wakati wa hafla hiyo, Naibu Gavana wa Kaunti ya Kiambu, Bi Joyce Ngugi ambaye ni mtaalam wa kisaikolojia, alisema serikali ya Kaunti ya Kiambu itajitolea mhanga kuona ya kwamba inawasaidia wale wote walio na shida ya msongo wa mawazo.

“Tunaelewa vyema kuwa hali ya maisha imekuwa ngumu kwa kila mtu na kwa hivyo ni vyema kushirikiana na wataalam ili kuwashauri watu hao,” alifafanua Bi Ngugi.

Alieleza ya kwamba wataalam wa kisaikolojia na madaktari watafanya kikao na Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro ili kupanga mikakati ya namna ya kuwashughulikia watu walio na msongo wa mawazo na maswala ya kifamilia.

Alitoa tahadhari kwa watu wale wanaowakosoa wale walio na shida za msongo wa mawazo.

“Ni vyema kumuelewa mtu kwanza kabla ya kujaribu kumkashifu kutokana na shida yake,” alifafanua Bi Ngugi.

Naye mtaalam wa kisaikolojia Dkt Susan Gitau, alisema wataalam wa masuala ya msongo wa mawazo wanapanga kujumuika pamoja ili kuona ya kwamba wanawapa ushauri ufaao wote walio na shida tofauti zinazoendana na msongo wa mawazo.

“Jambo hilo linastahili kuchunguzwa kwa makini kwa sababu kwa siku za hivi karibuni tumeshuhudia kesi nyingi za watu kujitoa uhai, jambo linalotia hofu katika jamii,” alisema Dkt Gitau.

Alisema huu ndio wakati mwafaka kwa wataalam wote wa kisaikolojia kutoka Kiambu kufanya kikao maalum na gavana Nyoro ili kujadili hali hiyo ambayo imeenea karibu kote nchini.

Alisema kwa miezi kadha iliyopita amezuru sehemu tofauti za nchi akitoa ushauri kwa familia nyingi zinazopitia hali ngumu ya maisha.

“Hata hivyo, ninatoa ushauri kwa wote waliohudhuria hafla hii wawe mstari ya mbele kutafuta ushauri badala ya kuamua kujitoa uhai,” alishauri Dkt Gitau.

Aliwashauri wanafunzi kutumia vyema muda walio nao kupata elimu ili wabuni ajira siku za usoni.

Bi Susan Njeri Waititu, ambaye ni mke wa marehemu Francis Waititu aliyekuwa mbunge wa Juja, aliwashauri wale wanaopitia mambo magumu kutafuta ushauri wa kisaikolojia ili wasije wakajidhuru maishani.

Alitoa mfano wakati mumewe alikuwa akiugua saratani ya ubongo kwa zaidi ya miaka miwili, alipitia mambo mazito kimawazo, lakini alipokea ushauri ndipo akawa na utulivu.

Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) imeshauriwa kuwashughulikia walimu wao kwa kuwatafutia wataalam wa kisaikolojia wakati wanapopitia hali ngumu ya maisha.

You can share this post!

Akana kupora hoteli

Mish analenga kushiriki fiamu za Hollywood