• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Washukiwa 15 wa mauaji kuendelea kusota rumande

Washukiwa 15 wa mauaji kuendelea kusota rumande

MAHAKAMA mjini Nyahururu imeruhusu maafisa wa polisi kuendelea kuwazuilia washukiwa 15 wanaohusishwa na mauaji ya mwanamume wa umri wa miaka 25 kwa siku tano zaidi ili kukamilisha uchunguzi.

Hakimu Mkuu wa mahakama ya Nyahururu Charles Obulisa aliipa idara ya upelelezi ya jinai ya Nyandarua Kaskazini ruhusa ya kuwazuilia 15 hao kwa siku tano zaidi ili kuwaruhusu wapelelezi kukamilisha uchunguzi wa mauaji ya Amos Gichuki mnamo Mei 15, mwaka huu.

Wapelelezi waliiambia mahakama kwamba wanaamini kuwa Gichuki aliuawa kwenye baa moja katika eneo la Suguroi, Kaunti ya Nyandarua na mwili wake ukapelekwa nyumbani kwake, ukawekwa kitandani, kumwagiwa asidi usoni na kufunikwa na blanketi.

Mwili wake uliooza ulipatikana nyumbani kwake wiki moja baadaye, mnamo Mei 21. Akitoa ombi mbele ya mahakama, afisa wa upelelezi alisema kuwazuilia watuhumiwa hao kwa siku tano kutaiwezesha afisi ya DCI kufanya uchunguzi na kukusanya ushahidi dhidi yao.

Afisa wa upelelezi na kiongozi wa mashtaka waliiambia mahakama kuwa kuzuiliwa kwa washukiwa hao pia kutaruhusu ukusanyaji wa sampuli za DNA na damu kutoka kwa washukiwa, kuzipima na kupata vielelezo muhimu kabla ya kuwawasilisha washukiwa hao mahakamani Jumatatu wiki ijayo.

Tayari watu 17 wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo la mauaji ambalo limewashtua wakazi wa kijiji cha Suguroi. Kesi hiyo itatajwa Juni 28, 2021 wakati mahakama itatoa mwelekeo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Covid-19: WHO sasa kuzindua kituo chakuunda chanjo Afrika

Mwanahabari wa KBC aporwa