• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wataalamu: Ushuru mpya utaumiza raia

Wataalamu: Ushuru mpya utaumiza raia

PETER MBURU Na MARY WANGARI

MAPENDEKEZO kuhusu jinsi serikali inapanga kumtoza mwananchi ushuru katika mwaka wa kifedha unaoanza Julai yatamwongezea uzito zaidi kimaisha, kutokana na ushuru zaidi atakaotozwa licha ya ugumu wa maisha uliopo.

Hii ndiyo fasiri ya wataalamu wa masuala ya ushuru katika Shirika la PriceWaterhouse Coopers (PWC), ambao wamekosoa mapendekezo kadhaa katika Mswada wa Fedha 2023, ya kutoza mwananchi ushuru zaidi, wakishikilia kuwa hakuna uhakika kuwa serikali itapata mapato zaidi kutokana na ushuru unaopendekeza kutozwa katika sekta muhimu nchini.

Jana Jumatatu, kiongozi wa Muungano wa Azimio One Kenya, Raila Odinga, alipinga Mswada huo uliopendekezwa na serikali ya Rais William Ruto akisema kuwa ni mzigo utakaowakandamiza Wakenya hata zaidi.

Kuu zaidi katika pendekezo hilo ni kupandisha ushuru wa mafuta kutoka asilimia nane hadi asilimia 16, wakisema uzito wake utasikika kote nchini na kwa kila mwananchi.

“Serikali imekua ikikusudia kutoza huu ushuru lakini ni ushuru ambao unaumiza kila mtu, iwe mwendeshaji wa bodaboda au mmiliki wa kiwanda. Tunatarajia kuwa gharama ya maisha itapanda kutokana na mabadiliko haya,” akasema Bw Job Kabochi, mtaalamu wa masuala ya ushuru PWC.

Bw Kabochi pia alikosoa pendekezo la kupandisha ushuru wa kutuma pesa kwa njia ya simu kutoka asilimia 12 hadi asilimia 15, ambao alisema unahatarisha kuzalisha mifumo mibaya ya kutuma pesa miongoni mwa Wakenya watakaohisi kuwa wanatozwa pesa nyingi ili kuwatumia wapendwa wao pesa.

“Wakenya watakaohisi kuwa ni ghali kutuma pesa kupitia njia za sasa za simu huenda wakavumbua mbinu yao ambayo huenda ikawa hatari,” akasema, akiongeza kuwa serikali inafaa kutambua kuwa kwa kuweka gharama ya kutuma pesa kwa njia ya simu kuwa nafuu, inawasaidia Wakenya wengi kuwa katika mfumo halali wa pesa.

Serikali pia hutumia mbinu hizo kuwatumia wananchi pesa za misaada, jambo ambalo wataalamu hao wanasema huenda ushuru huu ukaathiri mapato yao.

Wataalamu hao pia wamekosoa pendekezo la kutaka ushuru unaolipiwa kodi za nyumba kulipwa ndani ya saa 24, pamoja na ushuru wa huduma nyingine ambazo kwa kawaida haulipwi kwa mbinu za kiteknolojia. Vilevile, wamekosoa pendekezo la kutoza asilimia tatu ya mshahara wa wafanyakazi kuwekwa kwa hazina ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini – ambao utachanigwa na mwajiri na mwajiriwa- wakisema kuwa litazuia waajiri kukuza nafasi nyingi za kazi kwa kuogopa mzigo zaidi.

Pendekezo hilo ni kuwa mwajiri na mwajiriwa watachanga pesa hizo kila mwezi, na mchango wao wote hautazidi Sh5,000.

“Kuingizwa kwa ushuru huu na mwingine utapunguza pesa wanazopata waajiriwa na waajiri pia wataongezewa mzigo wa kuajiri, jambo linaloweza kupunguza nafasi za ajira,” akasema Bi Shreya Shah.

  • Tags

You can share this post!

Waliosaidiwa na Uhuru wamgeuka

DCI: Baadhi ya miili Shakahola haikuwa na viungo muhimu

T L