• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Watalii wapiga kona baada ya kuona barabara mbovu Mayungu

Watalii wapiga kona baada ya kuona barabara mbovu Mayungu

NA MAUREEN ONGALA

MENEJA wa hoteli ya watalii ya Malaika katika eneo la Mayungu mjini Malindi ameeleza kuwa kuwepo kwa barabara mbovu katika maeneo hayo kumekuwa ni changamoto kubwa katika sekta ya utalii.

Hali hiyo imechangia pakubwa kwa baadhi ya hoteli na mikahawa ya watalii eneo hilo la ufuo wa bahari, kukosa watalii wa ndani na nje ya taifa hili.

Akizungumza na wanahabari katika hoteli hiyo Bw Joseph Charo alisema watalii wengi wamekuwa wakibadili mawazo ya hoteli watakazokaa wanapokuwa katika eneo hilo la Malindi pindi tu wanapoona ubovu wa barabara ya Mayungu.

“Watalii wengi sana wanatoa malalamiko kuhusu barabara mbovu na tunapoteza wateja wengi kwa sababu hiyo,” akasema.

Bw Charo alisema kuwa katika siku za hivi majuzi, watalii 13 kati ya 15 waliokuwa wamejitengea nafasi katika hoteli hiyo ya Malaika eneo la Mayungu, walibadili mawazo yao na kuchangua hoteli mbadala, pindi walipobaini hali mbaya ya barabara.

Sehemu ya mbele ya hoteli ya Malaika eneo la Mayungu mjini Malindi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Aliendelea kusema kuwa changamoto hiyo imechangia zaidi ya wafanyakazi 20 kulazimika kusalia majumbani mwao bila ajira.

Aidha, aliongeza kuwa licha ya wadau wa utalii katika eneo hilo la Mayungu kuahidiwa kuwa ujenzi wa barabara hiyo utatekelezwa na serikali ya Kaunti ya Kilifi, hakuna dalili zozote za ukarabati ama hata ujenzi wa barabara hiyo, hali ambayo wanadai kuwa itachangia katika kuzorota kwa mapato ya hoteli zilizoko eneo la Mayungu.

“Ile ahadi waliotupa sasa zimepita siku nyingi lakini hatujaona dalili zozote za kukarabatiwa kwa barabara hiyo. Tunaomba wadadarukie suala hilo,” akasema.

Alitoa wito kwa serikali ya kaunti kushughulikia kwa haraka swala hilo la barabara na kuimarisha usalama wa maeneo hayo ya shughuli za kiutalii.

Hali mbovu ya barabara katika mji wa Malindi na Watamu imekuwa changamoto kwa muda huku wadau wakitaka swala hilo kushughulikiwa.

Malalamishi hayo yanatolewa huko Wakenya wakitarajia mvua ya El Nino inayotazamiwa kuanza mwezi huu wa Oktoba.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto aendelea kummegea Mudavadi tonge serikalini

Aliyepandikizwa nywele husubiri kati ya mwaka mmoja na...

T L