• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 7:05 PM
Rais Ruto aendelea kummegea Mudavadi tonge serikalini

Rais Ruto aendelea kummegea Mudavadi tonge serikalini

NA MARY WANGARI

RAIS William Ruto mnamo Jumatano usiku alifanyia mabadiliko ya ghafla Baraza la Mawaziri, hatua iliyoathiri mawaziri saba na makatibu wa wizara mbalimbali.

Katika hatua hiyo ambapo wizara kadhaa zilijumuishwa na kubadilishwa majina, Kiongozi wa Taifa vilevile alimwongezea mamlaka Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye sasa ataongoza Wizara ya Masuala ya Kigeni iliyokuwa ikiendeshwa na Waziri Dkt Alfred Mutua.

Miongoni mwa mawaziri waliohamishwa ni pamoja na Waziri wa Biashara Moses Kuria ambaye sasa ataongoza Wizara ya Utumishi wa Umma iliyokuwa ikishikiliwa na Waziri Aisha Jumwa ambaye sasa ndiye Waziri mpya wa Jinsia na Utamaduni.

Dkt Mutua amehamia Wizara ya Utalii iliyokuwa ikiongozwa na Bi Penina Malonza ambaye sasa amemrithi Bi Rebecca Miano kama Waziri wa Jumuia ya Afrika Mashariki

Bi Rebecca Miano sasa ndiye Waziri mpya wa biashara huku Waziri wa Maji, Alice Wahome akikabidhiwa Wizara ya Ardhi iliyokuwa ikiongozwa na mrithi wake Zacharia Njeru.

Wakati huo vilevile, Rais Ruto amemteua Seneta wa zamani Isaac Mwaura kama msemaji wa serikali kwa ushirikiano na mwanahabari Mwanaisha Chidzuga pamoja na mchanganuzi wa kisiasa Gabriel Muthuma kama manaibu wasemaji wa serikali.

Aidha, Rais Ruto ameteua na kubadilisha mabalozi 31 pamoja na manaibu mabalozi 14 kuwakilisha Kenya katika mataifa mbalimbali.

Kupitia notisi rasmi iliyofikia Taifa Leo, Rais alifafanua kuwa hatua hiyo inadhamiriwa kuanzisha mabadiliko muhimu yatakayohakikisha taasisi za serikali zimeimarishwa kutekeleza miradi mbalimbali ya serikali.

“Rais kwa kutumia mamlaka aliyotwikwa kama Kiongozi wa Taifa na Serikali kuambatana na Kifungu 132 cha Katiba, amefanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri,” ilisema taarifa iliyotumwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.

“Kufuatia hatua ya Rais, mabadiliko majukumu ya Wizara na Asasi za serikali yamebadilishwa. Hatua ya Kiongozi wa Taifa na Serikali imepanga upya Wizara, Asasi na Huduma za Kenya katika mataifa ya kigeni ili kuboresha utendakazi na kuimarisha utowaji huduma kuambatana na Manifesto ya ajenda ya Mabadiliko kuanzia Mashinani.”

  • Tags

You can share this post!

Pasta amenitunga mimba kisha akaniruka!

Watalii wapiga kona baada ya kuona barabara mbovu Mayungu

T L