• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Watu 300 wanaoishi na ulemavu Thika wapokea msaada

Watu 300 wanaoishi na ulemavu Thika wapokea msaada

NA LAWRENCE ONGARO

SHIRIKA la Hope Mobility Kenya limewafaa watu 300 wanaoishi na ulemavu kwa kuwapa viti vya magurudumu kwenye hafla iliyoandaliwa katika kanisa katoliki la St Patricks’ mjini Thika.

Katibu wa Idara ya Maswala ya Kijamii Bw Joseph Motari aliyekuwa mgeni wa heshima katika hafla hiyo, alisema serikali imejitolea mhanga kuwajali walemavu.

“Serikali tayari inafanya juhudi kuwalinda wakongwe, walemavu na mayatima, ili waishi maisha ya kisasa,” alisema katibu Motari.

Alitoa wito kwa wazazi kuwapenda wana wao ambao ni walemavu badala ya kuwatelekeza,” alisema Bw Motari.

Katibu wa Idara ya Maswala ya Kijamii Bw Joseph Motari. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alisema serikali itafanya juhudi kuona ya kwamba inawajali watu wanaoishi na ulemavu kote nchini.

“Hatutaki kuwe na ubaguzi wowote wakati wa kutoa usaidizi kwa watu wanaoishi na ulemavu,” alifafanua katibu huyo.

Alisema wiki ijayo, wakongwe waliogonga umri wa miaka 70 na zaidi watapokea Sh2,000 kila mmoja kwa kila mwezi.

Hatua kama hiyo pia itazingatiwa kuwafaa walemavu walio katika hali ngumu ya kujimudu kimaisha.

Mbunge wa Thika Bi Alice Ng’ang’a, alisema yeye kama mwenyekiti wa kamati ya maswala ya kijamii bungeni atahakikisha walemavu wanalindwa ipasavyo.

“Leo nimefurahi kuona ya kwamba walemavu kutoka eneo langu wananufaika pakubwa,” alisema mbunge huyo.

Alisema serikali itafanya juhudi kuona ya kwamba walemavu wanatendewa haki kwa kupewa msaada wowote unaohitajika.

Alisema atatumia mamlaka yake kuona ya kwamba anazuru maeneo yote ya nchi ili kutatua shida za walemavu.

Walemavu hao walinufaika na msaada wa chakula kutoka kwa mbunge huyo.

Walemavu hao walipokea unga wa mahindi kilo nne, mafuta ya kupika, mahindi kilo 18, ndengu kilo sita, na maharagwe kilo sita kwa kila mmoja.

Mkurugenzi wa shirika la Hope Mobility Kenya Bw Jack Muthui, alisema tayari wamezuru kaunti mbili kama Nakuru na Trans Nzoia na kusambaza viti vya magurudumu kwa walemavu.

“Tutaendelea kushirikiana na serikali kuona ya kwamba walemavu wanapata haki yao jinsi inavyotakikana,” alisema Bw Muthui.

Alisema kile wangeiomba serikali ni kulegeza ushuru wa kulipia vifaa vya walemavu vinavyoagizwa kutoka ng’ambo.

“Iwapo ombi hilo litatiliwa maanani, bila shaka fedha za kulipia ushuru zinaweza zikatumika kununua viti vingi vya magurudumu kuwafaa walemavu zaidi,” alifafanua mkurugenzi huyo.

  • Tags

You can share this post!

Azimio wazindua Paybill kuwafaa majeruhi, familia za wahanga

Mlima Kenya: Hongo ya Sh7m kwa siku ulevi utande bila...

T L