• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Mlima Kenya: Hongo ya Sh7m kwa siku ulevi utande bila maswali

Mlima Kenya: Hongo ya Sh7m kwa siku ulevi utande bila maswali

Na MWANGI MUIRURI

TAIFA Leo hii leo inakufichulia sakata ya baadhi ya polisi kushirikiana na wamiliki wa baa katika eneo la Kati ili kutoa idhini ya uvunjaji sheria na wakazi kulewa kupindukia.

Mtandao huu wa ufisadi ndio ambao Naibu Rais Rigathi Gachagua ameapa kupambana nao na kuuvunja lakini kinaya kikiwa ni kwamba, maafisa hao walio ndani ya ukora huo ndio wanaotakiwa kujimaliza.

Katika sakata hiyo, maafisa hao hudai Sh200 kwa siku kutoka kwa kila baa ili wamiliki na wahudumu wakikaidi sheria za kuhudumu, wasiwajibishwe kwenye mkondo wa sheria.

Zaidi ya Sh7 milioni hukusanywa kwa siku. Pesa hizo zinaweza kuwa nyingi kwa kuwa takwimu za ufisadi huwa haziwekwi wazi.

Mkuu wa Utawala eneo hilo Bw Fred Shisia hajaonekana hadharani akionyesha makali ya kujituma kuhakikisha janga hilo limekabiliwa vilivyo.

Hali hiyo ya ‘nipe hela nikupe idhini uleweshe watu’ kati ya maafisa hao na polisi ndiyo imesemwa kuchangia magonjwa, umaskini, kutojielewa kwa wengi na wengine kuishia kuwa bwege.

Wengine huaga dunia katika hali za kutatanisha, wakikabiliwa na msongo wa mawazo na kuishia kujitia kitanzi.

Mwanamume akiwa na msongo wa mawazo. PICHA | MAKTABA

Vile vile, hali hii imechangia kuenea kwa ubakaji, ulawiti na uvamizi kukita mizizi katika jamii hizo za eneo la Kati. Walioathirika zaidi ni wakazi wa kaunti za Kirinyaga, Murang’a, Nyeri, Nyandarua na Kiambu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa bodi ya kupambana na ulevi kiholela katika Kaunti ya Nyandarua Bw Joseph Kaguthi, hali si hali tena na ulevi unafaa kutangazwa kama janga la eneo la Kati.

Bw Kaguthi aidha ndiye alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Ulevi na Mihadarati (Nacada).

“Tuko na takriban baa 35,000 katika eneo hili ambazo zimesajiliwa. Ukijumlisha hata zile ambazo hazijasajiliwa, utapata idadi hiyo ikipanda. Habari tulizo nazo ni kwamba maafisa wa usalama hudai Sh200 kwa kila baa ili jicho la utekelezaji sheria lifumbwe. Hii inaelezea ni kwa nini utakumbana na walevi mijini na vijijini kwa wakati wowote ule licha ya sheria kukataa hilo,” akasema Bw Kaguthi.

Nao wamiliki wa baa wakishalipa hongo hiyo, huvuka mipaka ya uvunjaji sheria kwa kuruhusu wateja wao kuandamana na watoto wao wadogo wajumuike nao kushiriki ulevi ndani ya baa.

Alisema ukosefu wa uwajibikiaji sheria unazamisha familia nyingi kwa umaskini haswa baada ya wengi kuuza mali ili kupata pesa za ulevi.

Maafisa wa usalama wameripotiwa kuchukulia baa na magweni ya pombe haramu kuwa shamba lao la kuvuna vya bwerere.

Wengine hata wamewekeza katika biashara za ulevi na kwa kuwa wao ndio watekelezaji sheria, baa zao huwa hazifuati sheria.

Wanasiasa pia wakiwekeza katika biashara ya ulevi hushawishi mapendeleo kwa manufaa yao hivyo basi kuzua mwanya wa ukora wa kibiashara.

Kwa mujibu wa Bw James Kariuki ambaye ni mshirikishi wa mapambano dhidi ya ulevi kiholela miongoni mwa vijana, “serikali za kaunti zinazidi kutoa leseni kiholela ambazo hukiuka sheria kuu kuhusu udhibiti wa uuzaji vileo.”

Alisema kuwa serikali hizo hutoa leseni ambazo hupuuza masharti ya ulevi uafikiwe kati ya saa kumi na moja jioni hadi saa tano usiku katika siku za kawaida na kuanzia saa nane mchana mnamo wikendi na sikukuu.

“Nao maafisa wa utawala ambao wanafaa kupiga msasa operesheni za baa huingizwa katika mtandao wa kuvuna hongo ili kuifumbia macho sheria. Nao polisi ambao ndio wanafaa kutekeleza sheria na kuwakamata wanaokiuka na kisha kuwafungulia mashtaka hudai mgao wa keki ya hongo,” akasema.

Alisema kuwa kila wadi ya eneo hilo huwa na mpangilio maalum wa namna ya kuokota hongo hizo.

“Baadhi ya polisi hupendelea hongo hiyo kukusanywa na kuwasilishwa kila baada ya wiki moja huku wengine wakidai ipatikane kila siku. Kuna wale wamiliki wa baa ambao hupewa wajibu wa kukusanya hongo hizo na kuziwasilisha na hao ndio huwa kiungo thabiti cha kuhakikisha sheria za ulevi zimekiukwa,” akasema.

Wakati wowote vyombo vya habari vinajitokeza kumulika ukora huo, washirikishi wa sakata hiyo huwasilisha majina ya wenye baa na wahudumu ambao huwa hawatilii mkazo kuwasilisha hongo.

“Hao ndio hukamatwa na hatimaye wakifikishwa katika vituo vya polisi, wanahitajika kulipa ada za juu au wawasilishwe mahakamani,” akasema polisi mmoja ambaye alisema tusimtaje kwa sababu anaweza akahujumiwa na wakubwa wake kazini.

Bw Kaguthi anawashauri wenyeji katika maeneo ambayo yameathirika na ulevi kiholela wawe wakipasha serikali habari kupitia nambari spesheli ya 988.

“Katika usiri wako, wewe chukua simu yako na uanze ujumbe wako kwa kutaja kaunti uliyomo ukifuatisha na kaunti ndogo na kijiji au mtaa wako. Elezea kero yako na utume ujumbe huo kwa nambari 988 ambapo jina lako na nambari yako ya simu haitaanikwa,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Watu 300 wanaoishi na ulemavu Thika wapokea msaada

Udukuzi: Owalo asema data za Wakenya ziko salama

T L