• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Yaya anayeugua Ukimwi mashakani kwa kutemea mate chakula cha bosi wake kumuambukiza virusi

Yaya anayeugua Ukimwi mashakani kwa kutemea mate chakula cha bosi wake kumuambukiza virusi

JOSEPH NDUNDA NA SAMMY WAWERU 

MWANAMKE mwenye umri wa miaka 24 anayeugua Ukimwi na aliyetemea mate chakula cha mwajiri wake, ameshtakiwa kwa jaribio la kutaka kumuambukiza virusi vya ugonjwa huo hatari.

Mshukiwa huyo anayetoka Kaunti ya Vihiga, alinaswa na kamera ya siri (CCTV) akijaribu kutekeleza kosa hilo mnamo Oktoba 25, 2023 mtaani Eastleigh, Nairobi.

Akisomewa mashtaka yanayomkabili mbele ya Hakimu Mkuu katika Mahakama ya Makadara, Erick Mutunga, yaya huyo aliyetambulika kama PKH (si majina yake halisi), alituhumiwa kutemea mate mlo wa bosi wake akijua waziwazi ana virusi vya Ukimwi, kwa lengo la kumuambukiza.

Tendo hilo linaenda kinyume na kukiuka Kifungu cha 26 (a) cha Sheria ya Makosa ya Ngono (SOA) ya mwaka 2006.

Mshukiwa, hata hivyo, alikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mutunga.

Mwajiri wake alitambua kuhusu kitendo hicho cha aibu alipokuwa akirejelea kanda ya CCTV, ili kujua matukio ya siku kutwa.

Kijakazi huyo alitekeleza tendo hilo akiwa jikoni, ambapo alikuwa anamuandalia chakula.

Bosi huyo, ambaye korti ilimtambua kama mlalamishi HYA (si majina yake halisi), aliambia mahakama kwamba alipopitia kanda za awali za CCTV aligundua yaya huyo amekuwa akitemea mate vyakula alivyoandalia familia yake.

Aliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Pangani, Nairobi na askari walipomkamata na kupekua begi yake walipata tembe za ARVs, zinazotumika na wagonjwa wa Ukimwi kupunguza makali.

Aidha, polisi walitwaa dawa hizo na kanda za CCTV kabla ya kumtia nguvuni.

HYA aliambia askari waliofanya uchunguzi kwamba aliajiri PKH Oktoba 20, 2023 kupitia kituo cha ajenti kuandika vijakazi kilichoko South C, Nairobi.

Mshukiwa alikuwa amehudumu kwa muda wa siku tano pekee, na ilibainika amekuwa akiugua Ukimwi tangu utotoni mwake.

Upande wa mashtaka, uliomba korti kumzuia PKH katika Kituo cha Polisi cha Pangani ili apelekwe hospitali kwa uchunguzi zaidi wa kiafya.

Huku kisa cha yaya huyo kikiibua maswali chungu nzima kuhusu mienendo ya vijakazi, visa vya wafanyakazi wa nyumbani kushambulia waajiri wao na hata watoto hushuhudiwa mara kwa mara.

Baadhi, hulalamikia kupata ujira duni hasa maeneo ya mijini na wengine kudhulumiwa kikazi na kingono na mabosi wao wa kiume.

  • Tags

You can share this post!

Ten Hag aning’inia pembamba Man United wakiyumba...

Mtoto mvulana avalishwe ‘diapers’ au aachwe...

T L