• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Mtoto mvulana avalishwe ‘diapers’ au aachwe nyeti zake zipunge hewa?

Mtoto mvulana avalishwe ‘diapers’ au aachwe nyeti zake zipunge hewa?

NA WANGU KANURI

MJADALA wa iwapo mtoto wa kiume anapaswa kuvalishwa nepi (diaper) au la bado ungalipo huku wazazi mbalimbali wakiwa na maoni tofauti kuhusu mada hii.

Taifa Leo ilizungumza na kina mama ambao walieleza mtazamo wao walipoanza kuwavalisha wana wao nepi. Joy* anasema kuwa aliacha kumfunga mwanawe nepi akiwa na miezi saba ili sehemu zake za siri zipunge hewa.

“Tunamfunga tu anapolala au tukienda pahali ingawa kuosha nguo zake kila baada ya kujiendea haja si rahisi,” akasema.

Bi Joy anaeleza kuwa mtazamo huu ulitokana na kupenda kwa mwanawe kukaa bila nepi na pia kuogopa awe tasa sababu ya uume wake kutopata hewa ipasavyo.

Kwa upande wake Winnie Njeri, kutomfunga nepi mtoto wake wa kiume kulitokana na athari yake kwa ukuaji wa mwanawe. Anasema kuwa kutoka siku ya kwanza, mwanawe hakuwa anaenda haja akifungwa nepi.

“Nikimtoa nepi, alikuwa akienda haja vizuri. Nilipojaribu aina mbalimbali za nepi hazikumfaa. Tulipoenda hospitalini, nikaelezwa na daktari niache kumfunga diaper,” anasimulia.

Hata hivyo, Bi Njeri, alimfunga tu mwanawe usiku kinyume na ushauri wa daktari. “Alianza kufura sehemu zake za siri na ikabidi apashwe tohara. Baadaye nikaacha kabisa kumfunga diaper.”

Dkt Abdirahman Farah, mtaalamu wa watoto katika hospitali ya Royal London Polyclinic katika eneo la Parklands anasema kuwa ni muhimu kubadilisha nepi za watoto wa kike na wa kiume kila mara ili kumwepusha mtoto dhidi ya maambukizi na vipele vinavyotokana na nepi.

“Kinyesi huwa na chumvi pamoja na vitu vingine vyenye madhara ambayo hudhuru na kuumiza ngozi. Pia, kukiweka kinyesi hicho kwa muda mrefu huwa kunafanya bakteria na kovu (fungi) kuota kwa urahisi na kusababisha maambukizi kwa ngozi na viungo vingine vya uzazi,” anafafanua.

Hata hivyo, kuna uhusiano wa kutobadilisha diaper hizi mara kwa mara na kumhatarisha mtoto kupata maambukizi katika mfumo wa njia ya mkojo (Urinary Tract Infections).

Dkt Farah anafafanua, “Kinyesi kinaweza kusafiri hadi kwenye mrija wa mkojo (urethra) na kusababisha maambukizi ya njia hii ya mkojo (urine infection). Hata hivyo, jinsia zote mbili zipo katika hatari ya kupata magonjwa haya.”

Licha ya kumhatarisha mtoto kupata maambukizi ya njia ya mkojo, kutombadilisha nepi mara kwa mara kunaweza kumsumbua mtoto na hata kuathiri kukula na kulala kwake.

Vipele vya nepi husababishwa na kutobadilisha nepi mara kwa mara. Unyevunyevu wa haja yake unapokaa kwa muda mrefu pamoja na mabadiliko ya pH yaliyosababishwa na mkojo na kinyesi, huharibu ngozi ya mtoto.

Dkt Farah pia anaeleza kwamba makosa ya kawaida ambayo wazazi wanaweza kufanya kuhusiana na matumizi ya nepi ni kutumia saizi isiyofaa ya nepi. Saizi kubwa au ndogo sana huifanya haja kuvuja au kusababisha kuwasha kwa ngozi.

“Pili, kutobadilisha nepi au kumvalisha mtoto aina mbalimbali za nepi mara kwa mara, kutonawa mikono baada ya kubadilisha nepi, kuosha mtoto mara kwa mara kwa sabuni na hivyo kusababisha vipele na ukavu wa ngozi na kutotupa nepi ipasavyo ni baadhi ,” anaongezea.

Hali kadhalika, Dkt Farah anashauri kuwa mlezi au mzazi wa mtoto anapaswa kuzuru hospitali pindi tu akiona vipele kwenye ngozi ya mtoto wake, mmomonyoko wa ngozi (skin erosion) au akishuku kuwa kuna maambukizi kwenye mfumo wa mkojo.

Kama mwanawe Bi Njeri, Dkt Farah anashauri kuwa iwapo mtoto wako ametahiriwa, ni vyema kumpaka mafuta kwa wingi kwenye uume na eneo la kati ya makalio ili kuepuka mgusano.

“Mfunge diaper kwa wepesi ili kuepuka maumivu ya baada ya kupashwa tohara.”

Isitoshe, Dkt Faraha anaeleza kuwa wazazi wanaweza kusawazisha haja ya kumweka mtoto wao katika nepi na haja ya kuipa ngozi ya mtoto wao hewa safi kwa kumpa mtoto mapumziko ya kumfunga nepi kwa muda mfupi badala ya kumbadilisha kila mara anapojiendea haja.

“Vipele vya nepi vinaweza kuzuiwa kwa kubadilisha nepi mara kwa mara, kuosha eneo lililofunikwa na nepi hiyo kwa maji vuguvugu na kisha kupaka mafuta sehemu hiyo,” anashauri Dkt Farah.

Isitoshe, mzazi au mlezi wa mtoto huyo anapaswa kunawa mikono kabla na baada ya kubadilisha nepi. Anapompangusa, Dkt Farah anashauri kuwa ni vyema kupangusa mtoto kuanzia mbele kuenda nyuma badala ya kutoka nyuma kwenda mbele katika sehemu zake za siri.

Hatua hii humwepusha na kuchafua mrija wa mkojo unaoweza kuwa na kinyesi na hivyo kusababisha maambukizi ya mfumo wa mkojo.

  • Tags

You can share this post!

Yaya anayeugua Ukimwi mashakani kwa kutemea mate chakula...

Sababu kuu kufurushwa kwa Kawira kunaweka uoga viongozi wa...

T L