• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Afueni wakazi wa Chepkitale wakiahidiwa kituo cha polisi

Afueni wakazi wa Chepkitale wakiahidiwa kituo cha polisi

NA JESSE CHENGE

[email protected]

NI afueni kwa wakazi wa Chepkitale, kata ya Kaptama eneobunge la Mt Elgon baada ya Kamishna wa Kaunti ya Bungoma Thomas Sankei kutangaza kuwa serikali itajenga kituo cha polisi katika eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo wakati wa ziara yake, Sankei alisema kuwa kituo cha polisi kitasaidia kutatua changamoto nyingi za kiusalama katika maeneo ya mpaka wa Kenya na Uganda.

“Kituo hiki cha polisi hakitatatua tu migogoro ya mpakani lakini pia kitashughulikia visa vya ukosefu wa usalama ndani ya eneo hilo lote,” alisema.

Tangu uhuru, eneo la Chepkitale katika msitu wa Mt Elgon halijawahi kuwa na kituo cha polisi ambapo wenyeji wanaweza kuripoti visa vya ukosefu wa usalama.

Kutoka Chepkitale hadi kituo cha polisi kilicho karibu ni umbali wa kilomita 45.

Pia alikuwepo Mwakilishi wa Wadi (MCA) Hillary Kiptalam ambaye alisifu serikali kwa kuzingatia kuweka kituo cha polisi Chepkitale.

Kiptalam alitaja mtandao duni katika eneo hilo na kuomba serikali isaidie kusakinisha minara inayoboresha uunganishaji wa mtandao na mawimbi ya mawasiliano ya simu.

Kutokana na ukosefu wa kituo cha polisi katika eneo hilo, Kiptalam anasema kuwa baadhi ya raia wa Uganda wamekuwa wakitumia mwanya huo kuzua mtafaruku wakiwalenga wakazi wa Mt Elgon.

“Migogoro hii ya mpakani haifai wakati inapopatikana mara kwa mara, kwa hivyo wenyeji wanapaswa kuunga mkono hatua hii thabiti,” Kiptalam aliongeza.

Kiptalam pia alisema kuwa viongozi wa eneo hilo wamekuwa na mkutano wa kina na Kamishna wa Kaunti, manaibu wa Kamishna wa Kaunti, wasaidizi wa kamishna na Kamanda wa Polisi wa Bungoma Francis Kooli juu ya jinsi eneo hilo linavyoweza kupata usalama wa kutosha.

Cosmas Murunga, mzee kutoka jamii ya Ogiek alisifu serikali kwa kuzingatia kuweka kituo cha polisi akithibitisha kuwa wenyeji wataunga mkono hatua hiyo.

Murunga alibainisha kuwa wazee wamebainisha ardhi ambapo kituo hicho kitawekwa lakini kwa sasa watatumia makazi yaliyopo wakati bado wanangojea ununuzi wa serikali.

“Tayari tumebainisha nyumba ambapo maafisa wanaweza kuishi tunaposubiri ununuzi wa serikali. Inahitaji tu ukarabati mdogo,” Murunga aliambia Taifa Leo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kaunti ya Bungoma Bw Kooli alisema kuwa yuko katika ushirikiano na Kamishna wa Kaunti ya Bungoma na ofisi ya kitaifa ili kuhakikisha kuwa mahali hapo panajengwa kituo cha polisi ili kuleta huduma karibu na mwananchi.

  • Tags

You can share this post!

Mradi wa mabohari wa The Link kusaidia kuimarisha uchumi

KRU yashusha bei ya tiketi kutoka Sh300 hadi Sh100 kujaza...

T L