• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
KRU yashusha bei ya tiketi kutoka Sh300 hadi Sh100 kujaza Nyayo

KRU yashusha bei ya tiketi kutoka Sh300 hadi Sh100 kujaza Nyayo

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga Kenya (KRU) limetangaza kupunguza bei ya tiketi za kuingia ugani Nyayo jijini Nairobi kwa siku ya mwisho ya mashindano ya raga ya dunia ya wachezaji 15 kila upande wasiozidi umri wa miaka 20 hapo Julai 30.

Katika juhudi za kujaza uwanja huo unaobeba mashabiki 30,000, KRU imekata bei ya tiketi ya kawaida kutoka Sh300, ambazo mashabiki walilipa Julai 15, Julai 20 na Julai 25 wakati wa mechi za makundi, hadi Sh100.

Zoezi la kuuza tiketi kwa bei hiyo mpya kupitia nambari USSD *805#, lilianza Julai 26 na litafungwa Julai 29 saa sita usiku.

Mashabiki watakaoamua kununua tiketi siku ya mechi (Julai 30) watalipa Sh300 langoni kushuhudia mataifa manane yakipimana ubabe kuorodheshwa kutoka nafasi ya kwanza hadi mwisho.

Tiketi za watu mashuhuri ni Sh1,000 nao wanafunzi wa shule za msingi na upili waliovalia sare ya shule wataruhusiwa kuingia uwanjani bila kulipa ada yoyote.

Mwenyekiti wa KRU, Alexander Sasha Mutai ameomba wapenzi wa raga wajitokeze kwa wingi kuwapa wachezaji wa Kenya U-20 (Chipu) msukumo watakapovaana na mabingwa wa Afrika (Barthes Trophy) Zimbabwe kuamua nafasi ya tano na sita.

“Mchuano huo utakuwa wa mwisho wa Chipu. Ni muhimu kwa Chipu, taifa la Kenya na sisi wote kwa sababu itaamua nani ndiye mbabe barani Afrika. Pia, tutapata bingwa wa dunia wa daraja la pili siku hiyo,” amesema Mutai.

Uruguay na Uhispania walioshinda makundi A na B, watalimana katika fainali, huku mshindi kati yao akipandishwa ngazi hadi mashindano ya dunia ya daraja la kwanza.

Scotland na Samoa watapepetana kuamua nambari tatu na nne nao Hong Kong na Amerika watamenyana kutafuta nafasi ya saba na nane.

Mkurugenzi wa KRU wa Masuala ya Biashara, Harriet Okach amesema kuwa bodi hiyo mpya ya KRU imejitolea kufanya kila iwezalo kubadilisha raga nchini Kenya na kufikisha mchezo huo katika kiwango kingine.

Nyota wa zamani wa Afrika Kusini, Tendai ‘The Beast’ Mtawarira na rais wa Shirikisho la Raga Afrika Herbert Mensah ni baadhi wageni wakuu watakaofika uwanajni siku ya mwisho ugani Nyayo.

Mensah atawakilisha rais wa Shirikisho la Raga Duniani, Sir Bill Beaumont, katika kupeana tuzo kwa mabingwa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa mashindano hayo ya dunia jijini Nairobi, Ian Mugambi ameomba Wakenya wachukue fursa ya bei ya tiketi kupunguzwa kujaza uga wa Nyayo.

Kenya ilichapwa 28-7 na Zimbabwe katika fainali ya Afrika mwezi Aprili ugani Nyayo kwa hivyo italenga kulipiza kisasi.

  • Tags

You can share this post!

Afueni wakazi wa Chepkitale wakiahidiwa kituo cha polisi

Msimu wa 2022-23 Ligi ya Divisheni ya Kwanza wanawake...

T L